ACT-Wazalendo waitaka Serikali kufuta sheria zinazobana uhuru wa vyombo vya habari

Waziri Kivuli wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi wa chama cha ACT Wazalendo, Philbert Macheyeki.

Muktasari:

  • Chama cha Act Wazalendo kimeitaka Serikali kufuta sheria zote zinazopora uhuru wa vyombo vya habari huku wakitaka mapitia ya sheria hizo uwe shirikishi.

Dar es Salaam. Chama cha Act Wazalendo kimeitaka Serikali kufuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya Habari na kutengeneza sheria mpya kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sekta ya Habari.

Pia kimeitaka Serikali kusimamia uanzishwaji wa Baraza huru la habari nchini ili kulinda na kutetea haki na maslahi ya wanahabari.

Hayo yameelezwa kupitia uchambuzi wa bajeti ya Wizara Ya Habari, Mawasiliano Na Teknolojia Ya Habari Kwa Mwaka Wa Fedha 2023/2024 uliofanywa na waziri kivuli wa sekta hiyo kutoka ACT-Wazalendo, Philbert Macheyeki.

Kwa mujibu wa taarifa ya uchambuzi iliyotolewa na chama hicho inaeleza kuwa, tangu nchi ipate Uhuru, tasnia ya habari imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zinatokana mfumo wa utamaduni kandamizi.

Utamaduni kandamizi umepelekea Serikali kutunga sheria za habari zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa habari.

“Sheria hizo hizo ni kama vile, Sheria ya Magazeti ya 1976, Sheria ya Usalama wa Taifa 1977, Sheria ya Mawasiliano ya kieletroniki na Posta 2010, Sheria za makosa ya kimtandao 2015 (Cybercrimes Act 2015), Sheria ya takwimu 2015,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alisema, katika taarifa ya utekelezaji wa bajeti mwaka 2022/2023 Serikali imeeleza kuwa imeanza kufanya mapitio ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambapo muswada wa marekebisho ya Sheria hiyo ulisomwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Februari, 2023.

“Ingawa, Serikali imeonyesha nia ya kufanya mapitio lakini kuna ushirikishwaji mdogo sana juu ya sheria hiyo. Bado zipo sheria nyingine kandamizi kwa ustawi wa tasnia ya habari nchini,”imesema taarifa hiyo.

Kufuatia suala hilo waliitaka Serikali, iongeze ushirikishwaji katika mchakato wa mapitio ya Sheria ya huduma ya habari na muswada uliowasilishwa Bungeni mwezi Feb 2023 upelekwe kwa wadau na kujadiliwa kwa kina.