Afariki dunia baada ya kuzama Ziwa Victoria

Muktasari:
Jumla ya watu watatu ndani ya kipindi cha miezi mitatu mwaka huu wamezama ndani ya Ziwa Victoria eneo la fukwe za Gymkana mjini Bukoba.
Bukoba. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera limeopoa mwili wa kijana anayesadikika kuwa na miaka kati ya 14 na 15 Mkazi wa Wilaya ya Ngara aliyekufa maji baada ya kwenda kuogelea katika Ziwa Victoria eneo la Gymkana kata ya Miembeni Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Mwili wa kijana huyo ambaye hajafahamika majina, umeopolewa leo Ijumaa Septemba 15, 2023 kisha kupelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba kwa ajili ya kuutambuliwa.
Afisa Habari wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Sajenti Shabani Mussa amesema tukio la kuzama kwa kijana huyo lilitokea Septemba 14 saa 8:00 mchana akiwa na kijana mwingine Muganyizi Longino (12) ambaye pia alizama lakini akaokolewa na watu waliokuwa eneo hilo.
“Marehemu ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Ngara amepoteza maisha jana baada ya kuzama juhudi za kuanza kutafuta mwili wake zilianza ambapo mwili umepatikana leo na kuweza kuopolewa kisha kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya taratibu za uchunguzi na kupelekwa kuhifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba,”amesema Mussa
Mwananchi digital imezungumza na kijana aliyenusurika, Muganyizi Longino (12) ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Karagwe nakudai kuwa siku ya tukio yeye na marehemu walikutana kituo cha mabasi Bukoba nakupanga safari ya kwenda kuogelea kwenye fukwe za Ziwa Victoria.
Amesema walifika eneo la fukwe na kuanza kuogelea ndipo maji yaliwazidi uwezo ila kwa bahati, vijana waliokuwa karibu na eneo hilo wakawahi kumuokoa huku mwenzake maji yalimzidi nguvu na kumpeleka mbali nakusababisha vijana wale kushindwa kumuokoa.
Esta Sypilian Mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba amewatahadharisha wazazi na walimu kuwa walinzi wa watoto majumbani na shuleni kwa kuwazuia kwenda kuogelea eneo hilo.
Naye Ofisa Uvuvi Mkoa wa Kagera, Efrazi Mkama amesema kwa sasa hali ya hewa ziwani ni ya upepo mkali hivyo akiwataka wavuvi na watumiaji wa maji kuchukua tahadhari akiongezea kuwa Serikali imeishapiga marufuku watu kwenda kuogelea katika fukwe hizo za Manispaa ya Bukoba.