AfCHPR yapata jaji mpya
Jaji Dennis Adjei akiapa mbele ya Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa majaji wa mahakama hiyo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Jaji huyo, Dennis Adjei kutoka nchini Ghana ameapishwa leo Agosti 29, mbele ya Rais wa mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud kuwa miongoni mwa Majaji 11 wa Mahakama hiyo.
Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imepata jaji mpya kutoka nchini Ghana, Jaji Dennis Adjei baada ya aliyekuwepo kumaliza kipindi chake cha miaka sita.
Jaji Adjei ameapishwa leo Jumatatu Agosti 29 mbele ya Rais wa mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud ambapo anachukua nafasi ya Jaji Marie Theresa Mukamulisa anayerudi nchini Rwanda baada ya kumaliza muda wake.
Mahakama hiyo ambayo inaundwa na majaji 11 raia wa nchi wanachama wa umoja wa Afrika ilianza shughuli zake rasmi mwaka 2006 mjini Addis Ababa na baada ya mwaka mmoja ikahamia kwenye kiti chake cha kudumu Jijini Arusha.
Akizungumza baada ya uapisho huo, Jaji Imani amesema mahakama hiyo imepata jaji atakayeleta mawazo mapya katika kuhakikisha shughuli za mahakama zinafanikiwa kwa kiwango cha juu.
"Tunategemea kunufaika katika michango yake katika kuboresha shughuli za kimahakama, uwezo wake utaweza kuleta mawazo mapya na kupelekea mahakama katika ngazi nyingine ya kuhakikisha haki zinaendelea kuzingatiwa katika bara la Afrika," amesema
Wakati akila kiapo, Jaji Adjei amesema kama mjumbe wa mahakama hiyo atahakikisha anafanya kazi kwa uaminifu na kwa uadilifu mkubwa na kwamba hatatoa siri za mahakama hiyo.
Akimzungumzia Jaji huyo, Msajili wa mahakama hiyo, Dk Robert Eno amesema Jaji Adjei ana utaalamu mwingi na anatambulika katika nyanja mbalimbali za sheria katika mahakama za Afrika.
"Jaji Adjei amesoma chuo kikuu cha Ghana na ana shshada ya sheria, shahada ya uzamivu katika masuala ya utawala katika chuo kikuu cha Uingereza, shahada ya uzamili katika masuala ya makosa ya jinai na anatambulika katika nyanja mbalimbali za kisheria katika mahakama hii ya Afrika," amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema serikali inatambua mchango wa mahakama hiyo na kwamba chombo hicho cha mahakama kimekuwa kukitetea haki za binadamu na kwamba ni chombo muhimu.
"Kuteuliwa kwako ni heshima katika mahakama hii pamoja na nchi unayotoka,hii inaonyesha ni jinsi gani unaaminiwa kama msimamizi wa haki za watu.
"Sisi kama serikali tutaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha shughuli za mahakama hazikwami na ndio maana serikali imetenga eneo lenye hekta 25 katika eneo la Laki laki ili kuhakikisha mnakuwa na jengo la mahakama la kudumu," amesema.