AG ataka maboresho sheria ya madai

Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Eliezer Feleshi.
Muktasari:
- Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi ametaka maboresho ya sheria ya mwenendo wa madai sura 33.
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Jaji Eliezer Feleshi amependekeza maboresho ya sheria ya mwenendo wa madai sura 33, ili iruhusu kusajiliwa kwa shauri mahakamani mara itakapothibitika limepitia ngazi za usuluhishi na kushindikana.
Jaji Feleshi ameyasema hayo jijini Ddodoma leo, Februari 1, 2023 alipozungumza katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria Duniani.
Amesema pamoja na kuundwa jopo linaloshughulikia kupatikana kwa waendesha usuluhishi na tayari 494 wameshapatikana, lakini idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na mahitaji.
“Uhalisia uliopo leo ni kwamba, ukiondoa migogoro yenye asili ya madai iliyoko kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba na mahakama za mwanzo, yapo mashauri zaidi ya 15,000 ya madai ya aina mbalimbali ambayo hayajaisha katika mahakama za mahakimu na zile za juu yake,” amesema.
Kutokana na hilo, ameeleza ni vema yafanyike maboresho katika sheria ya mwenendo wa madai sura ya 33 ili shauri lipate sifa ya kusajiliwa mara baada ya kuthibitisha kuwa limepitia ngazi za usuluhishi na ukashindikana.
Hata hivyo, amesema ofisi yake itasimamia matakwa ya sheria ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na tayari alishaelekeza, watendaji waweke kipaumbele kumaliza migogoro kwa njia hiyo.