Ahadi ya Gambo yawakuna wafanyabiashara Arusha

Muktasari:

Changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika soko kuu jijini Arusha imepata ufumbuzi baada ya mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo kutekeleza ahadi ya kuchimba kisima cha maji.

Arusha. Changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika soko kuu jijini Arusha imepata ufumbuzi baada ya mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo kutekeleza ahadi ya kuchimba kisima cha maji.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, Mwantumu Shabani amesema utekelezaji wa ahadi hiyo utawasaidia wafanyabiashara na wananchi wanaozunguka eneo hilo kupata maji ya uhakika.

"Tunamshukuru mbunge wetu kwa kutekeleza ahadi kwa wakati kutokana na soko kuwa na mwingiliano mkubwa ambao unahitaji upatikanaji wa maji safi na salama muda wote ili kuhakikisha usalama wa afya za wananchi," amesema Mwantumu.

Amesema maji safi na salama kwa wafanyabiashara ni muhimu hasa bidhaa za matunda zinahitaji usafi ili kuwahakikishia walaji usalama wa afya zao.

Diwani wa Kati, Abdulrasul Tojo amempongeza  Gambo kwa kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Amesema licha ya Gambo kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kutatua kero za wananchi bado anaendelea kuwa kimbilio na tumaini kwa wananchi waliomchagua.

"Wananchi wa jimbo la Arusha Mjini wameonyesha kufurahishwa na utendaji kazi wa mbunge wetu kwa kujielekeza kwenye vitendo zaidi ikiwa ni pamoja na kuwa sauti ya wananchi wa jiji la Arusha," amesema Tojo.

Kabla ya kuchimba kisima cha soko kuu, Gambo alianza kuchimba kisima cha soko la Kilombero ambalo ni moja ya masoko makubwa yanayopokea mazao kabla ya kusambazwa masoko mengine.