Ahueni kwa wananchi Serikali inavyoimarisha huduma za afya

Muktasari:
Miongoni mwa sababu za kuongezeka umri wa kuishi kwa Mtanzania kutoka miaka 67 na miezi mitatu mwaka huu hadi miaka 74 ifikapo mwaka 2035 ni uboreshwaji wa huduma za afya.
Miongoni mwa sababu za kuongezeka umri wa kuishi kwa Mtanzania kutoka miaka 67 na miezi mitatu mwaka huu hadi miaka 74 ifikapo mwaka 2035 ni uboreshwaji wa huduma za afya.
Hali hii inaakisi katika bajeti kuu ya Serikali iliyopitishwa hivi karibuni na kuanza kutekelezwa Julai mosi, kwani Serikali imeonyesha nia ya kuendelea kuboresha sekta hiyo kwa kuongeza miundombinu, vifaatiba, dawa pamoja na wataalamu.
Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ugubuyu anasema uboreshwaji wa huduma za kijamii na nyingine ni moja ya sababu za kuongezeka kwa umri wa wananchi.
“Huduma za afya zikiimarika pamoja na nyingine ni mojawapo ya kichocheo cha kuongezeka kwa umri wa kuishi,” anaeleza.
Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria nchini kwa mwaka 2015- 2016 (TDHS- MIS) unaonyesha, vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 51 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai hadi kufikia 43.
Miongoni mwa changamoto zinazotajwa kuchangia ongezeko la vifo kwa watoto ni ukosefu wa huduma za afya zenye kiwango kinachostahili na ukosefu wa vifaatiba.
Hivi karibuni Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali alisema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya afya, kukarabati na kupanua miundombinu ya kutolea huduma ya afya, ikiwemo ujenzi wa Hospitali Maalumu ya Mama na Mtoto jijini Dodoma.
Ameahidi Serikali kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Magharibi, kukamilisha upanuzi wa hospitali nane za rufaa za mikoa na ujenzi wa hospitali hizo katika mikoa mipya mitano ya Katavi, Njombe, Songwe na Simiyu.
Pia kuboresha huduma za matibabu ya ubingwa bobezi katika Hospitali ya Taifa na Kanda kwa kuimarisha miundombinu na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba. Dk Ugubuyu anasema katika utoaji wa huduma za afya maeneo makuu yanayozingatiwa ni ufikiwaji wa huduma, kumudu gharama za matibabu, huduma zinazozingatia viwango pamoja na uzingatia wa usawa katika huduma.
Anasema kwa kipindi kirefu ndani ya sekta ya afya uwekezaji umekuwa ukifanyika maeneo ya mijini.
“Uwekezaji wetu mkubwa ulikuwa Arusha, Dar es Salaam na Mwanza kuliko eneo lingine lolote katika nchi yenye watu milioni 60. Unatoa huduma katika mikoa minne pekee, hii ilikuwa ni kunyima haki na fursa watu wengine,” anaeleza.
Kwa kuimarisha huduma ndani ya hospitali za rufaa za mikoa anasema, kunaipa Tanzania nafasi ya kuwa na huduma sawa katika mikoa yote nchini. “Wananchi wetu wametofautiana kipato, maana yake huduma hizi watu walikuwa na uwezo wa kuzipata katika hospitali binafsi, wasio na kipato hawapati kokote kwa sababu serikalini hazipo na hawawezi kumudu gharama za sekta binafsi,” anaeleza.
Anasema uwekezaji unaofanywa na Serikali, unamfanya kila Mtanzania bila kujali uwezo wake kiuchumi kupata huduma.
Kuhusu ubora wa huduma, Dk Ugubuyu anaeleza uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye miundombinu na vifaa tiba.
“Tunakwenda kuziona hospitali zote za rufaa za mikoa zikiwa na CT Scan, mwanzoni tulikuwa na CT Scan nane nchi nzima kwa hospitali za Serikali kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma,” anaeleza.
Anasema hali hiyo inamaanisha ni mikoa hiyo pekee ndio watu walikuwa na uwezo wa kupata huduma, mingine walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.
Kuhusu rasilimali watu, Dk.Sichalwe anasema kwa mwaka huu Serikali imetenga Sh8 bilioni kuwasomesha watumishi katika sekta ya afya na inaendelea kuinisha mahitaji ya watumishi, kuomba kibali cha ajira pamoja na kuendelea kuajiri watumishi kwa mikataba.
Kwa upande wake, Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe anasema uanzishwaji wa Hospitali Maalumu ya Mama na Mtoto jiji Dodoma itakuwa faraja kwa wanawake wengi, hasa wenye changamoto za uzazi.
Hata hivyo, anasema ipo changamoto kwa hospitali hiyo kujengwa Dodoma pekee, kwani matarajio ya wananchi wengi ni kupata huduma za namna hiyo ndani ya mikoa yao.
Hii ni kutokana na kile anachobainisha gharama zitakuwa kubwa kwa mwananchi mwenye matatizo ya uzazi kufunga safari kufuata huduma za kipekee zinazotolewa Dodoma kupitia hospiali hiyo.
Akizungumzia hospitali hiyo maalumu, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichawale anasema ujenzi wake utakuwa wa mfano nchini na Afrika Mashariki na Kati na kwamba zimetengwa Sh8 bilioni kwa ajili kuwasomesha wataalamu wa ndani na nje ya nchi.
Mtaalamu wa Maabara kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Alex Mlwisa anasema uboreshaji wa miundombinu kutasogeza huduma kwa wananchi, hali itakayochangia kukuza uchumi zaidi badala ya kutumia muda mrefu kufuata huduma.
Dominick Hosea, mkazi wa Tabata anasema uhakika wa wananchi kupata huduma za afya hupunguza vifo kwa kuwa mgonjwa anafikishwa hospitali kwa wakati na kupatiwa huduma.
Anasema ni jambo jema Serikali kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya afya, kwani itaepusha vifo vinavyotokana na kukosa huduma kwa wakati.