Aiba mtoto wa bosi wake, adaiwa kumlawiti kwa miezi mitano

Muktasari:

  • Kijana huyo aliyekuwa anafanya kazi ya kuchunga mifugo kwa bosi wake Simioni Abel huko wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, alitoroka na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 14 aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Miwaleni na kuja kuishi naye mkoani Arusha.

Arusha. Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Lebahati (35-37) anatuhumiwa kumtorosha mtoto wa kiume wa bosi wake na kwenda kuishi naye kinyumba kwa miezi mitano mfululizo huku akimlawiti.

 Kijana huyo aliyekuwa anafanya kazi ya kuchunga mifugo kwa bosi wake Simioni Abel huko wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, alitoroka na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 14 aliyekuwa akisoma Shule ya Msingi Miwaleni na kuja kuishi nae mkoani Arusha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wazazi wa mtoto huyo, walisema kuwa kijana huyo alitoroka tangu mwezi wa pili ambapo aliiba mbuzi 35 na kwenda kuuza kabla ya kuja kuondoka na kijana wao.

"Siku ya tukio mwishoni mwa mwezi wa pili Lebahati aliondoka nyumbani asubuhi kama kawaida kwenda kuchunga ng'ombe na mbuzi na sisi kuendelea na harakati zetu lakini kurudi jioni tukakuta mbuzi 35 hakuna na kijana wetu hayupo na kwenye simu hapatikani," alisema baba wa mtoto huyo Simioni Abel.

Alisema kuwa katika kumtafuta kila mahala baadae mtuhumiwa alipatikana na katika mawasiliano alikana kuondoka na mtoto huku akidai aliondoka na kuacha mifugo shambani.

"Tulimtafuta mtoto hadi tulikata tamaa kabisa lakini wiki iliyopita alipiga simu na kudai alikuwa na mtoto na  kunitaka nikampokee eneo la Kawawa mjini Moshi kuwa amempakiza basi, nilifanya hivyo na kwenda kumchukua bila kujua kuwa alikuwa na matatizo yoyote kwani yeye mwenyewe hakusema chochote zaidi ya kulala hovyo akisema anajisikia vibaya," amesema.

Alisema kuwa baada ya wiki moja walipigiwa sim kutoka kwa mtendaji wa Kata ya Kisongo mkoani Arusha kuwa mtoto wao anahitajika kwa uchunguzi na matibabu zaidi kutokana na alilawitiwa.

"Jambo hilo nilishtuka nikaamua kumshirikisha mdogo wangu tuliyekuwa tunapambana nae katika jambo hilo ndio tukafunga safari kuja Arusha baada ya taarifa hizo na tulipofika hadi hospital ikabainika kweli mtoto aliingiliwa kinyume na maumbile," amesema baba wa mtoto huku akiangua kilio.

Akizungumzia tukio hilo, mtoto huyo anasema kuwa kijana huyo alianza kumfanyia vitendo hivyo mjini Moshi siku za mwisho wa wiki walipokuwa wanaenda kuchunga mifugo, kabla ya siku ya tukio walipoiba mifugo na kwenda kuuza mnadani na kutoroka naye kuja Arusha.

"Alianza kunifanyia huko Moshi porini tukienda kuchunga na kunipa hela huku akinitishia nikisema ataniua. Hata siku ya kutoroka alipeleka mbuzi mnadani na kunitaka nimsindikize akisema anakuja kwao Arusha kusalimia lakini baada ya kufika hakuniruhusu kutoka na badala yake akawa ananifanyia vitendo hivyo kila siku kwa kuniziba mdomo na akitoka ananifungia ndani," amesema.

Akizungumzia tukio hilo, Mtendaji wa Kata ya Kisongo, John Nkini alisema kuwa walipata taarifa za kijana huyo kuishi na mtoto wa kiume kinyumba na walimkamata kwa mahojiano na kukana kuhusika hivyo waliamuachia na ndipo alipotoroka.

"Tulipata fununu za taarifa hizi na tulimkamata mtuhumiwa na kumuhoji lakini alikanusha hivyo tulimuachia ili kufanya kwanza mawasiliano ya upande wa pili ambao ni wazazi wa mtoto kuthibitisha tukio hilo na baadaye walipokuja na kuthibitika mtoto aliingiliwa kijana huyo alikimbilia kusikojulikana hadi sasa," amesema Nkini.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justin Masejo amesema kuwa tukio hilo wanalishughulikia.

"Asante kwa taarifa naomba kushughulikia," amejibu.

Baba mdogo wa mtoto huyo, Ramadhani Laswai amesema kuwa baada ya vipimo mtoto wao amebainika kuathirika sehemu za haja kubwa kutokana na kuingiliwa.

"Mtoto amekutwa ameharibika, hasa mishipa ya sehemu za haja kubwa hazina nguvu kabisa yaani zimelegea," amesema.

Alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuingilia kati swala hilo kumsaka mtuhumiwa ili hatua Kali za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.

"Tunaomba Serikali na waziri mwenye dhamana kuingilia kati swala hili kwani juhudi za kumsaka mtuhumiwa ni ndogo sana, wiki nzima hakuna mafanikio na wahusika hawasemi chochote na ukizingatia walimkamata awali na kumwachia bila sababu ya msingi, kiukweli tumeumia mtoto wetu kufanyiwa kitendo hiki," amesema.