Ajikata uume wake akidai kuchoshwa na ugonjwa

New Content Item (1)
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumzia tukio la mwanaume kujikata sehemu zake za siri kwa kile alichodai kuchoshwa na ugonjwa unaomsumbua miaka mitano sasa. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Marko Samwel (32), anadaiwa kujikata na kuzinyofoa sehemu zake za siri kwa madai ya kuchoshwa na maradhi yanayomsumbua ambayo hata hivyo hayajawekwa wazi.

Mwanza. Mkazi wa kijiji cha Kibitilwa kata ya Ilula Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Marko Samwel (32) anatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi baada ya kujikata na kuondoa kabisa uume wake kwa kutumia kisu.

Samwel anadaiwa kujifanyia kitendo hicho cha kikatili Mei 3 mwaka huu Saa 7 usiku kwa madai kuwa amechoka kuuguza maradhi yanayomsumbua (yamehifadhiwa) kwa zaidi ya miaka mitano.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema mwanaume huyo alijikata kwa kutumia kisu kisha kuziondoa kabisa sehemu zake za siri jambo lililosababisha apoteze damu nyingi na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kabla yakupatiwa rufaa ya kwenda Bugando anakoendelea na matibabu.

"Amekata uume wake kwa kisu kikali kwa madai kwamba amechoka kuugua, akakimbizwa Hospitali ya wilaya ya Kwimba lakini hali yake ikazidi kuwa mbaya akakimbizwa Bugando,"

"Hali yake inaendelea vizuri na sisi tunaendelea kumsubiria apone kabisa arejee kwenye utimamu wake ili atueleze kwa nini amekata sehemu zake za siri baada ya hapo tutamfikisha Mahakamani," amesema Mutafungwa

Mutafungwa ameitaka jamii kuepuka kuchukua maamuzi yanayoweza kuwaathiri kimwili na kisaikolojia akitolea mfano tukio hilo na kuwataka wenye changamoto kuwahusisha ndugu, wanasaikolojia na viongozi walioko katika maeneo yao.