Akata rufaa kupinga mama wa kambo kusimamia mirathi
Muktasari:
Mkata rufaa amedai kuwa uteuzi wa mama yake wa kambo, Fatuma Mohamed haujawahi kusikilizwa na mahakama yoyote Tanzania na hukumu ya kumteua mjibu rufaa huyo haijawahi kutolewa na mahakama kuwa ndiye msimamizi wa mirathi.
Dar es Salaam. Abdullatif Hamisi amemkatia rufaa mama yake wa kambo, Fatuma Mohamed akipinga uteuzi wake wa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yake Mohamed Hamisi Abdallah kwa kuwa hakuwahi kujaza fomu ya kuomba kuteuliwa na kwamba uteuzi wake haukuwahi kusikilizwa na mahakama yoyote Tanzania.
Shauri hilo la mirathi namba 41 la mwaka 2023 lilikuja kwa ajili ya kutajwa mbele ya Naibu Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kuhusu Masuala ya Kifamilia (ndoa, talaka na mirathi), Temeke, William Kaaya.
Hamisi amekata rufaa hiyo akidai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Temeke katika kituo hicho jumuishi ilikosea kisheria na kimantiki kusema kuwa Fatuma aliteuliwa na mahakama wakati hakuwahi kujaza fomu namba moja ya kuteuliwa kuwa msimamizi.
Alidai kuwa uteuzi wa Fatuma haujawahi kusikilizwa na mahakama yoyote Tanzania na hukumu ya kumteua mjibu rufaa huyo haijawahi kutolewa na mahakama kuwa ndiye msimamizi wa mirathi.
"Fomu namba nne inayohusiana na kudai, kukusanya na kulipa madeni ya marehemu aliyokuwa anadaiwa akiwa hai iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Temeke katika kituo hicho haijawahi kutolewa na Hakimu yeyote Tanzania aliyemteua Fatuma kuwa msimamizi wa mirathi," alidai Hamisi
Katika rufaa hiyo pamoja na mambo mengine, alidai kuwa mahakama imekosea kisheria na kimantiki akieleza kuwa msimamizi wa mirathi hakuwa anatekeleza amri za mahakama kwa sababu alikuwa na kesi nyingi zilizokuwa zikiendelea.
Alidai kuwa mazingira na hali halisi katika kumbukumbu za mahakama Fatuma ndiye aliyekuwa akikata rufaa na kuanzisha kesi mbalimbali Ili kukwepa utekelezaji wa amri ya mahakama.
Katika rufaa hiyo anadai mahakama hiyo ilikosea kisheria na kimantiki kutoa maamuzi kwamba kulikuwa na kesi nyingi zilizozuia usimamizi wa mirathi kutojaza hati ya mali zilizokusanywa wakati mazingira yanaonyesha kuwa tangu mwaka 2006 alipoteuliwa hapakuwa na kesi yeyote mahakamani.
Pia alidai kuwa Fatuma hakuwahi kujaza fomu namba tano na sita zinazohusiana na maombi ya kujaza mali na madeni aliyokusanya, kugawa mali za marehemu kwa warithi na kufunga mirathi.
Hivyo Hamisi amedai kuwa kutokana na hayo ameiomba Mahakama Kuu Kituo Jumuishi ifutilie mbali sehemu ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Temeke kwa kuwa Fatuma hajawahi kuteuliwa na Mahakama yoyote Tanzania kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu Mohamed Abdallah.
Pia ameiomba mahakama hiyo kumuamuru Fatuma arudishe mahakamani nyaraka zote na fedha alizokusanya kwa kuwa alitakiwa awasilishe ndani ya miezi minne.
Kadhalika, anaiomba Mahakama hiyo imtengue Fatuma kuwa msimamizi wa mirathi kwa kuwa amekaidi amri zote alizopewa na mahakama huku akimbagua Hamisi.
Shauri hilo litasikilizwa Novemba 10, 2023 baada ya kuahirishwa kwa kuwa Jaji Rwizile Kalichumba ambaye awali alipangiwa kulisikiliza amehamishwa kikazi.