Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Akatwa mguu, aomba msaada wa mguu bandia

Mlemavu wa mguu, Hassan Suwapanga akizungumza wakati wa mahojiano na mwandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha ya Hellen Hartley

Muktasari:

  • Wahenga walisema kabla hujafa hujaumbika. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Hassan Suwapanga, maarufu kama Kurwa Bonge aliyepata changamoto ya kukatwa mguu wa kulia baada ya kukanyaga glasi iliyovunjika na kutupwa katika uwanja wa nyumba yao, tukio hilo lilibadili kabisa mwelekeo wa maisha yake.

Dar es Salaam. Wahenga walisema kabla hujafa hujaumbika. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Hassan Suwapanga, maarufu kama Kurwa Bonge aliyepata changamoto ya kukatwa mguu wa kulia baada ya kukanyaga glasi iliyovunjika na kutupwa katika uwanja wa nyumba yao, tukio hilo lilibadili kabisa mwelekeo wa maisha yake.

Akisimulia mkasa uliosababishwa kukatwa mguu, anasema siku hiyo majira ya alfajiri mvua kubwa ilinyesha katika eneo la Mbezi Makabe anakoishi ambako kuna changamoto ya upatikanaji maji, hivyo alishawishika kutoka nje kukinga maji ya mvua.

Alisema kuwa alipokuwa akiendelea kukinga maji alimuona nyoka, jambo lililomtia hofu na kukimbia kuelekea ndani, lakini kabla hajafika alikanyaga kipande cha glasi iliyovunyika.

Alieleza kuwa kutokana na hofu aliyokuwa nayo hakuhisi maumivu yoyote wakati huo, lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda alianza kuhisi maumivu yaliyokuwa yanaendelea kuongezeka.

“Siku ya pili eneo nililojichoma palikuwa pagumu mno, hali iliyonitia hofu na kuamua kwenda hospitali iliyopo jirani, baada ya uchunguzi daktari alisema eneo hilo limetengeneza usaha hivyo ninahitajika kufanyiwa operesheni ndogo ili kuuondoa,” alisema Hassan.

Hata hivyo, alisema kuwa hata baada ya kufanyiwa operesheni hiyo hakupata nafuu, badala yake alianza kuona ngozi ya mguu mguu ikibanduka.

Alisema baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuendelea kupatiwa matibabu kisha kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambapo baada ya uchunguzi ilionyesha mguu huo umeanza kuoza, hivyo ikashauriwa ukatwe, pia iligundulika kuwa ana ugonjwa wa kisukari.

“Ilikuwa ngumu kukubaliana na suala hilo, lakini ilinilazimu kukubaliana nalo ili kuokoa maisha yangu,” alisema.

Alisema baada ya kukatwa mguu maisha yake yalibadilika, kwani awali alikuwa akifanya kazi ya ujenzi, lakini sasa mambo yamebadilika.

“Siwezi tena kufanya kazi za ujenzi kama awali, kwa sababu ninashindwa kutembea umbali mrefu nikiwa na magongo.

“Nimeamua kufanya biashara ninazoziweza nikiwa nyumbani, ikiwemo kushona viatu pamoja na kuuza kahawa ili kupata fedha za kujikimu kimaisha,” alisema.


Aomba msaada

Hassan pamoja na mambo mengine, aliomba msaada wa kupatiwa mguu bandia ili aweze kuendelea na kazi yake ya ujenzi kwa ufanisi kama ilivyokuwa awali.

“Ninaamini nitakapopatiwa mguu bandia nitaweza kuendelea na shughuli zangu kama kawaida na kuihudumia familia yangu kama awali,” alisema.

Unaweza kumsaidia Hassan kwa kutumia namba 0783348614 iliyosajiliwa kwa jina la Mariam Suwapanga au piga simu kwa mhariri wa Mwananchi, zilizopo kwenye gazeti hili.