Akaunti benki ni suluhisho kutopotea fedha za Vicoba

Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi kutoka Absa Benki Tanzania, Heristraton Genesis
Muktasari:
- Miongoni mwa faida zinazobainishwa kwa vikundi kuhifadhi fedha zao benki ni pamoja na uhakika wa usalama wa fedha, kunufaika na riba inayolipwa kila baada ya muda fulani, kuongezeka kwa uwazi kwa wanachama pamoja na kupatia elimu ya fedha.
Dar es Salaam. Wanavikundi mbalimbali vya kijamii wamehimizwa kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyumbani kwa kuwa njia hiyo si salama, badala yake watumie benki ili kujiongezea faida na kukuza mitaji ya kibiashara.
Hayo yamemebainishwa leo Februari 13, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Benki ya Absa Tanzania, Ndabu Swere katika hafla fupi ya uzinduzi wa akaunti maalum kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya kijamii ijulikanayo kama ‘Absa Group Saving Account’.
Swere amesema mara kadhaa kumekuwa kukiripotiwa matukio ya fedha kupotea au watunza hazina na viongozi wa vikundi vya Vicoba kutumia fedha za wanachama wenzao jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya kikundi husika.
“Ili kuepusha matukio kama hayo kujitokeza ni vyema wanachama ni vyema kuhifadhi fedha zao benki ambapo pamoja na kuwahakikishia usalama wa fedha zao lakini kuna faida nyinginezo ambazo kikundi kinaweza kunufaika,” anaeleza.
Amesema ili kutatua changamoto hiyo ya upotevu wa fedha hizo za vikundi wao kama taasisi ya fedha waliona kuna haja ya kuja na huduma itakayowawezesha wanavikundi mbalimbali vya kijamii kuweka fedha huku kukiwa na uwazi kwa wanachama wote wa kikundi husika.
“Kupitia akaunti hiyo ya kikundi, vikundi mbalimbali kuanzia ngazi ya familia kuweka fedha huku wanachama wakiweza kupata taarifa mbalimbali kuhusu fedha walizoweka ikiwemo nani ametoa pesa, kiasi gani kimewekwa na sasa kiwango gani cha pesa kimefikiwa.
“Ili kupata huduma hiyo kikundi husika kinatakiwa kuhakikisha kina katiba inayotumika katika kukiendesha, barua ya utambulisho, muktasari wa kikundi pamoja na wanachama walioteuliwa kwa ajili ya uwekaji wa sahihi,” anaeleza.
Ameongeza kuwa pamoja na kuwekeza wao kama taasisi ya fedha wanawapatia wanakikundi husika elimu ya kifedha itakayowasaidia kufanya uwekezaji sahihi wa fedha zao.
Naye Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi kutoka benki hiyo, Heristraton Genesis amebainisha faida mbalimbali ambazo vikundi vinaweza kuipata ikiwa watahifadhi fedha zao benki.
Miongoni mwa faida alizobainisha Genesis ni pamoja na kunufaika na riba ambayo kikundi kitaipata katika kipindi cha muda fulani, urahisi wa kupata mikopo katika benki pamoja pamoja na kupatiwa elimu ya fedha ambayo itawasaidia katika uwekezaji wa pesa zao.