Alama za kudumu za Magufuli Mwanza
Muktasari:
- Jana wakazi wa Mwanza waliaga mwili wa Hayati John Magufuli katika Uwanja wa CCM Kirumba na katika barabara mbalimbali ulizopita huku wakikumbuka alama ambazo ameuachia mkoa huo.
Mwanza. Juzi wakazi wa Mwanza waliaga mwili wa Hayati John Magufuli katika Uwanja wa CCM Kirumba na katika barabara mbalimbali ulizopita huku wakikumbuka alama ambazo ameuachia mkoa huo.
Msafara wenye mwili wake ulianzia Uwanja wa Ndege Mwanza hadi Kirumba ambako ilifanyika ibada na kisha kuelekea mkoani Geita.
Madaraja ya juu Furahisha, Kigongo-Busisi
Ujenzi wa daraja la juu la waenda kwa miguu la Furahisha lililogharimu zaidi ya Sh4.7 bilioni ni moja ya kumbukumbu ya kudumu ya Magufuli kwa wakazi wa Mwanza.
Fedha za kujenga daraja zilitokana na uamuzi wake kusitisha sherehe za Muungano za mwaka 2016.
Ujenzi wa daraja hilo lililozinduliwa Oktoba 30, mwaka 2017, umemaliza matukio ya ajali za barabarani zilioangamiza maisha ya wengi eneo la Furahisha lenye pilikapilika nyingi, hasa nyakati za asubuhi na jioni kutokana na shughuli na huduma kadhaa za kijamii.
Japo bado liko katika hatua za awali, ujenzi wa daraja la JPM katika Ziwa Victoria kuunganisha eneo la Kigonga wilayani Misungwi na Busisi wilayani Sengerema kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni ni alama nyingine ya kuduma aliyoacha Mwanza.
Litakapokamilika, daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 litakuwa ndilo refu kuliko zote ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Miradi mingine itakayokumbukwa ni ujenzi wa soko (Sh20 bilioni) na stendi kuu ya jijini Mwanza ya zaidi ya Sh14 bilioni.
Wakazi wa Manispaa ya Ilemela pia wameachiwa kumbukumbu ya stendi ya kisasa ya mabasi na maegesho ya malori katika eneo la Nyamhongolo unaogharimu zaidi ya Sh28 bilioni.
Usafirishaji majini
Katika sekta ya usafirishaji, Magufuli ameacha kumbukumbu ya kuduma kama kukarabati meli ya Mv Victoria kwa zaidi ya Sh22 bilioni.
Pia hawatasahau ukarabati wa meli ya Mv Butiama kwa zaidi ya Sh4.9 bilioni na ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza unaoendelea katika bandari ya Mwanza Kusini kwa zaidi ya Sh89 bilioni.
Pia amewaachia kivuko cha Mv Ukara II cha Sh4.2 bilioni na kingine cha Mv Ilemela kilichogharimu zaidi ya Sh2.7 bilioni.