‘Aliyoyafanya Magufuli yalikuwa kiu ya Watanzania’
Muktasari:
Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk Halid Salum Mohammed amesema mapokezi ya wananchi katika miji mbalimbali ambayo mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu John Magufuli ulipita ni dhahiri kuwa aliyoyafanya enzi za uhai wake yalikuwa kiu ya Watanzania.
Dar es Salaam. Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk Halid Salum Mohammed amesema mapokezi ya wananchi katika miji mbalimbali ambayo mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu John Magufuli ulipita ni dhahiri kuwa aliyoyafanya enzi za uhai wake yalikuwa kiu ya Watanzania.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Machi 25, 2021 katika uwanja wa Magufuli wilayani Chato wakati akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kutoa salamu za pole katika shughuli za kuaga mwili wa kiongozi huyo.
“Amefanya mengi katika nchi hii na ushahidi ni yale yaliyotolea katika vituo vyote tulivyopita na mwili huu, wananchi wamejitokeza kwa ari kubwa na hiyo ni ishara tosha amefanya mambo ambayo wananchi tuliyahitaji. Kilichopo tudumishe ushirikiano kwa maana hayo ndiyo aliyoyajenga tuwe na ari ya kuijenga nchi yetu,” amesema.
Dk Mohammed alisema tayari wamefanikiwa kukamilisha asilimia 90 ya shughuli hiyo na haikuwa kazi rahisi.
“Leo ni kuaga kwa ajili ya wananchi wa mkoa huu na mikoa jirani, tulianza salama na tumefika salama kesho tutaupumzisha mwili huu katika nyumba yake ya milele,” amesema