Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magufuli na kauli kongwe ya ‘Tanzania ni masikini’

Magufuli na kauli kongwe ya ‘Tanzania ni masikini’

Muktasari:

  • Miongoni mwa changamoto zinazokabili nchi za Afrika ni kuwa na viongozi wanaotumia fedha na rasilimali za umma kujinufaisha wao, familia na washirika wao.

Miongoni mwa changamoto zinazokabili nchi za Afrika ni kuwa na viongozi wanaotumia fedha na rasilimali za umma kujinufaisha wao, familia na washirika wao.

Viongozi hao huapa kwamba wataongoza nchi kwa kujali masilahi ya wananchi, lakini wanapoingia ikulu, wanakuwa ni wasaliti namba moja wa raia wao.

Wale ambao hujipambanua kuwa upande wa wananchi tena wale wanyonge, ni ‘bidhaa adimu’ katika Bara la Afrika na hiyo ni moja ya sababu ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, kuzua hofu miongoni mwa Watanzania wakihoji ‘Tanzania itakuwaje bila Magufuli’.

Alikuwa ni kiongozi jasiri, mwenye uthubutu wa aina yake katika utekelezaji wa shughuli na majukumu yake ya kiserikali, aliliongoza Taifa tangu 2015, hadi alipofariki dunia Machi 17, mwaka huu, kwa maradhi ya moyo.

Tangu Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961 na baadaye mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, na mwaka huohuo nchi mbili hizo kuungana na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwelekeo umekuwa ni ujenzi wa taifa linalojitegemea.

Kila awamu ya uongozi wa serikali ikaimba Tanzania ni nchi inayofuata siasa ya ujamaa na kujitegemea, lakini kivitendo ujenzi wa nchi ukawa unategemea huruma za wafadhili kwa miaka mingi.

Ilifika mahali hata vyoo katika baadhi ya shule vimetokana na ufadhili na kuandikwa vimejengwa kwa hisani ya wa watu wa taifa fulani huko duniani, hii siyo sawa.

Rais Magufuli alipoingia madarakani, pasipo kigugumizi aliwaambia Watanzania nchi yao ni tajiri isiyostahili kuwa ombaomba wa misaada kutoka Ulaya, Marekani au kwingineko, katika kujenga taifa linalojitegemea.

Ilikuwa ni nadra sana pale anapozungumza na Watanzania ama katika mikutano ya hadhara kumaliza hotuba au mazungumzo bila kusema ‘Tanzania ni taifa tajiri lenye rasilimali chekwa.’

Magufuli ambaye kabla ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi alikuwa waziri kwa miaka 20 katika wizara tofauti, aliwathibitishia Watanzania kuwa nchi yao ni tajiri, kwa serikali aliyoiongoza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea fedha za wafadhili.

Shirika la Ndege la Tanzania ambalo wakati Magufuli anaingia madarakani lilikuwa na ndege moja mkweche, ni miongoni mwa mashirika ya umma yaliyofufuliwa kupitia utajiri wa rasilimali za taifa.

Kwa mfululizo, kwa kutumia fedha za Watanzania, ndege zikanunuliwa kirahisi mithili ya mama aendaye gengeni kununua nyanya na vitunguu.

“Sisi siyo masikini, nchi hii ni tajiri, Tanzania ni tajiri ndugu zangu, mniamini mimi,” ndivyo Magufuli alivyokuwa akisema na kurudia mara kwa mara, lengo likiwa ni kufuta imani iliyokuwa imejengwa na kujengeka vichwani mwa wanachi tangu uhuru, kuwa nchi yao ni masikini.

Siyo Tanzania tu, hata nchi za Afrika, kwa miaka mingi wananchi wameaminishwa na wanaendelea kuaminishwa kwamba mataifa yao ni masikini, huku ikifahamika hakuna bara tajiri kwa rasilimali kama Afrika.

Miaka mitano na miezi takribani minne ya uongozi wa Magufuli, hakuna kiongozi au mtendaji serikalini aliyefungua kinywa kuwaambia Watanzania miradi ya maendeleo haitekelezeki kwa sababu nchi ni masikini, au wafadhili hawajatoa fedha kama walivyoahidi.

Kauli ya Tanzania ni nchi masikini imetoweka na ile ya Tanzania ni tajiri kuziba pengo, huku miradi mikubwa ya maendeleo ikitekelezwa huku na kule nchini kote.

Wala rushwa na mafisadi, wezi na wabadhirifu wa mali ya umma, walitumia kauli ya Tanzania ni masikini kama uchochoro wa wao kuwanyonga wananchi wanyonge.

Uongozi wa Magufuli ulipokaza sheria dhidi ya uhalifu huo na kuchukua hatua pasipo kumuonea haya mtu, pamoja na kufuta mikataba ya kinyonyaji iliyokuwa ‘ikihomola’ rasilimali za nchi, Watanzania wakaanza kuamini Rais Magufuli alisema kweli, nchi siyo masikini.

Mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, uhujumu uchumi na ubadhirifu wa mali ya umma, yakawezesha fedha kupatikana kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi ya maendeleo inayomnufaisha kila Mtanzania. Hata pale alipohisi huenda kuna Watanzania wana wasiwasi wa ukamilikaji wa baadhi ya miradi kutokana na ukubwa wake, kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), aliwahakikishia itakamilika kwa sababu nchi ni tajiri.

Ni katika uongozi wa Magufuli, Watanzania wakang’amua kwamba fedha na rasilimali za taifa zilikuwa ‘zikipigwa’ kwa kiwango kisichomithilika kupitia uchochoro wa ‘Tanzania ni nchi masikini’.

Kwa muda mrefu, utumishi wa umma umekuwa ukichukuliwa kuwa ‘mradi’ kwa viongozi na watendaji waandamizi serikalini na katika mashirika ya umma kujinufaisha wao, familia na washirika wao, huku wananchi wakiachwa katika lindi la ufukara wakishindwa hata kupata mlo mmoja kwa siku. Baadhi ya viongozi na watendaji waandamizi serikalini walidiriki kuingia mikataba ya hovyo yenye mianya ya kutorosha nje ya nchi rasilimali kwa mtindo wa kifisadi wa ‘teni pasenti’ za mabilioni ya fedha. Kwa mfano, kiongozi anafahamu rada ni chombo muhimu kwa usalama wa nchi, lakini ufisadi unamtoa ufahamu na utu. Mfano mwingine, nchi inakuwa katika hatari ya kukumbwa na giza totoro kutokana na hali mbaya ya Shirika lake la Umeme (Tanesco), viongozi na watendaji serikalini wanalazimisha kampuni ya kwenye ‘brifukesi’ ipatiwe tenda, na ikapewa kweli. Wizi mtupu!

Hadi Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015, Tanesco ilikuwa hoi bin taabani mikataba ya ‘kirichimondi’ iliyokuwa ikimaliza kodi za Watanzania kwa faida ya viongozi wachache na ‘mabwana’ zao wa ndani na nje ya nchi.

Kiongozi fisadi wa nchi ya Afrika, anahujumu rasilimali za taifa lake na kwenda kuficha fedha benki za Ulaya, na kuwekeza vitega uchumi huko ughaibuni, hii ni akili kweli?

Hata baada ya kupatikana kwa uhuru kwa zaidi ya miaka 60, bado kuna nchi za Afrika zenye hospitali zisizo hata na ‘panado’ na wanafunzi hawana madawati.

Imeandikwa na Jacqueline Liana