Alinayedaiwa kuua kwa kukusudia, aiomba Mahakama umwachie huru

Muktasari:

  • Ndage anadaiwa kumuua Beatrice Onesmo kwa kumchoma kisu tumboni baada ya rafiki yake kupiga kelele zinazoashiria kuwa yeye ni mwizi.

Dar es Salaam. Mkazi wa Mkwajuni, Ismail Ndage (27) ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imsamehe na imwachiee huru, baada ya kukiri shtaka la kuua

 Ndage anadaiwa kumuua Beatrice Onesmo kwa kumchoma kisu tumboni baada ya rafiki yake kupiga kelele zilizoashiria kuwa yeye ni mwizi.

Mshtakiwa huyo amewasilisha ombi hilo leo Alhamisi, Novemba 24, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi za mauaji, baada ya kukiri shtaka lake la kumuua Beatrice kwa kukusudia kwa sababu alikuwa anajihami baada ya kuitiwa kelele za mwizi.

Mshtakiwa ametoa maelezo hayo, muda mfupi baada mahakama kumkuta na kesi ya kujibu.

Mshtakiwa huyo amekutwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wa mashidi wawili waliouwasilisha mahakamani hapo dhidi yake.

Akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili Harrison Lukosi, Ndage amedai kuwa siku ya tukio wakati akielekea soko la Tandika, mvua ilianza kunyesha iliyompelekea kusimama pembezoni mwa nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke aliyefahamika kwa jina la Editha Alphonce hivyo mwanamke huyo alianza kumvuta mkono kwa nguvu na kufanikiwa  kumuingiza ndani kwake kisha akamtaka kujamiana nae kwa malipo ya shilingi 3000.

Ndage amedai baada ya kukataa kufanya tendo hilo la ndoa, Editha alimtaka ampe Sh 2,000 kwa madai ya kuwa ameingiza mchanga ndani ya nyumba yake, ambapo mshtakiwa alikataa.

Wakati Ndage akiendelea kukataa ndipo Editha alipoanza kupiga kelele za kuashiria kuwa yeye ni mwizi huku akiwaita wamasai ambao ni walinzi wa eneo lile.

Ndage amedai ili kujiokoa kutoka mikoni mwa Editha ambaye alikuwa amenikumbatia kwa nguvu, alichukua kisu kilichokuwa kwenye beseni na kumchoma begani kisha akamsukuma na kufanikiwa kutoka nje na kukimbia.

"Wakati natoka nje nilikuta na kundi la watu walioanza kunimkimbiza miongoni mwao alitokea mwanamke aliyefahamika kwa jina la Beatrice Onesmo, ambaye alijaribu kunizuia ili anikamate, ndipo nilipomchoma kisu kwenye mgongo na mimi niliendelea  kukimbia," amedai Ndage.

Mshtakiwa huyo ambaye hasikii vizuri aliendelea kuieleza Mahakama alifanikiwa kukimbia na kurudi nyumbani kwake huko Mkwajuni ambapo aliendelea na majukumu yake mengine hadi Mei 20, 2018 alipokamatwa na askari akiwa anakunywa pombe za kienyeji katika kilabu ambacho hakutaja jina lake.

Mshtakiwa baada ya kumaliza kujitetea, Hakimu Mazengo, ameahirisha kesi hiyo hadi Disemba 7, 2022 kwa ajili ya kutoa   hukumu.

Katika kesi ya msingi, mshitakiwa huyo alidaiwa kutenda kosa hilo, Mei 14, 2018 eneo la Azimio lililopo Tandika wilaya ya Temeke.

Inadaiwa siku hiyo, katika eneo hilo, mshtakiwa anadaiwa kumuua Beatrice Onesmo kwa kumchoma kisu tumboni.