Aliyemwagiwa tindikali kupelekwa India kutibiwa

Muktasari:

Wakati Tariq Awadhi (31) akifikisha siku 55 akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) baada ya kumwagiwa tindikali familia yake wameiomba Serikali na Watanzania kumchangia ili aweze kupelekwa nchini India kupata matibabu kutokana na hali yake kuendelea kuwa mbaya.

Moshi. Wakati Tariq Awadhi (31) akifikisha siku 55 akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) baada ya kumwagiwa tindikali familia yake wameiomba Serikali na Watanzania kumchangia ili aweze kupelekwa nchini India kupata matibabu kutokana na hali yake kuendelea kuwa mbaya.

Tariq anahitaji Sh35 milioni ili aweze kupelekwa Hospitali ya Apolo iliyopo nchini India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa macho.

Tariq alifikwa na madhila hayo ya kumwagiwa tindikali Machi 5 mwaka huu wakati akitokea nyumbani kwake Shant town mjini Moshi kwenda sehemu ya kula chakula cha jioni ambapo akiwa njiani vijana wawili wakiwa na bodaboda walimmwagia kitu kinachodhaniwa kuwa ni tindikali usoni na mikononi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Aprili 30, 2022 mama mdogo wa Tariq, Magdalena Kessy amesema hali yake ni mbaya na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia aweze kwenda India kupata matibabu.

Pamoja na kumwomba Rais Samia, amewaomba pia Watanzania wenye kuwachangia ili waweze kumpeleka Tariq kwenye matibabu kutokana na hali yake kuwa mbaya.

"Jamani familia tumefika mahali tumeshindwa tunamwomba Mama Samia aweze kutusaidia ili tuweze kufanikisha matibabu ya Tariq maana hali yake ni mbaya, juzi alikuwa afanyiwe upasuaji hapa KCMC lakini kutokana na hali yake kuwa mbaya upasuaji ukashindikana,sasa tunatakiwa kumpeleka Hospitali ya Apolo  India kwa ajili ya matibabu zaidi,"

"Tumeambiwa na madaktari wa hapa KCMC endapo tukimuwahisha nchini India angalau anaweza kuona na zinahitajika Sh35 milioni kwa ajili ya matibabu,tunawaomba Watanzania walioguswa na Tariq watasaidie chochote walichonacho  maana bado ni kijana mdogo na ndoto zake bado hajatimiza,"amesema

Aprili 19 mwaka huu Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema wanamshikilia mtuhumiwa aliyemwagia Tariq tindikali na kwamba alikiri kutenda kosa hilo. 

Kwa yeyote atakayeguswa kumchangia kijana huyo, namba zake ni 0764510774 Au Akaunti namba zake ni: 3012111594790 Equity Benki kwa jina la Tariq Kipemba