Aliyerejeshwa kazini na Majaliwa aondolewa kupisha uchunguzi

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa mji Ifakara, Francis Ndulane amemuondoa John Mvanga kuwa kaimu mkuu wa kitengo cha Teknolojia, Habari na  Mawasiliano (Tehama) kupisha uchunguzi  kuhusu miamala ya mfumo wa mapato wa ofisi yake.

Morogoro. Mkurugenzi wa mji Ifakara, Francis Ndulane amemuondoa John Mvanga kuwa kaimu mkuu wa kitengo cha Teknolojia, Habari na  Mawasiliano (Tehama) kupisha uchunguzi  kuhusu miamala ya mfumo wa mapato wa ofisi yake.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Oktoba 4, 2019 Ndulane amethibitisha kuondolewa kwa Mvanga.

Septemba 16, 2019 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa mjini Ifakara wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro katika ziara ya siku tano alizungumza na watumishi wa mji huo na kumrejesha Mvanga baada ya kupata taarifa kuwa alihamishwa katika  halmashauri hiyo.

Mvanga alidaiwa kuhamishwa baada ya kubaini ubadhilifu wa fedha zilizotokana na makusanyo mbalimbali na Majaliwa alitaka arejeshwe mara moja na kutobughudhiwa.

 

Ndulane amelieleza Mwananchi kuwa Mvanga ataendelea na majukumu yake kama ofisa Tehama daraja la pili na si mkuu wa kitengo kwa sababu anadaiwa kufanya mambo yaliyosababisha hasara katika halmashauri hiyo.

Amesema amechukua uamuzi huo ili kutoingia katika makosa ambayo mwisho wake wangeshindwa kujitetea.

“Kwa sababu mamlaka za juu zimetaka tutekeleze kwa asilimia mia moja kwa hiyo tumemwandikia barua hiyo na kumpa hayo majukumu yake ili likitokea la kutokea mamlaka za juu zenyewe zitatusaidia kujibu,” amesema Ndulane.

Barua kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mji ya Oktoba Mosi, 2019 kwenda kwa Mvanga yenye kumbukumbu namba IFTC/CPF/IT/19/21 inaeleza kumuondoa kwenye nafasi ya kaimu mkuu wa kitengo cha Tehama, nafasi aliyoteuliwa kuishika Septemba 7, 2018.

“Kutokana na ofisi yangu kuendelea na uchunguzi wa miamala katika mfumo wa mapato ambayo ilifutwa na baadaye kurejeshwa bila idhini yangu, kuanzia tarehe ya barua hii nimekuondoa kwenye nafasi ya kukaimu kitengo tajwa hapo juu ili ofisi iendelee na uchunguzi.”

“Hautaruhusiwa kuingia kwenye mfumo wa mapato wa halmashauri mpaka ofisi yangu itakapokueleza vinginevyo majukumu yako ya ofisa Tehama daraja la pili yatabaki kama yalivyo katika barua yako ya kubadilishiwa muundo,” inasema sehemu ya barua  hiyo.