Aliyewekewa fuvu katika mtihani mpya baada ya matibabu

Muktasari:

  •  Baada ya mateso ya takribani miaka minane, matibabu ya upasuaji wa kubadilisha fuvu bandia la kichwa aliyopewa Marwa Msyomi (30) kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) yamebadili maisha yake kwa kumwondolea maumivu na mateso aliyokuwa akiyapata hapo awali.

Dar es Salaam. Baada ya mateso ya takribani miaka minane, matibabu ya upasuaji wa kubadilisha fuvu bandia la kichwa aliyopewa Marwa Msyomi (30) kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) yamebadili maisha yake kwa kumwondolea maumivu na mateso aliyokuwa akiyapata hapo awali.

Kwa mara ya kwanza Februari 28 gazeti la Mwananchi liliandika habari kuhusu kijana huyu na masaibu aliyokuwa anayapitia kutokana na hali yake ya kiafya ambapo MOI ilielekeza mgonjwa huyo afikishwe hospitalini hapo kwa matibabu.

Marwa alifanyiwa upasuaji huo Machi 9 mwaka huu baada ya kukaa muda mrefu bila tiba, hivyo fuvu bandia alilowekewa awali kupata maambukizi.


Kauli ya MOI

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MOI, Patrick Mvungi alisema walimpokea Marwa Februari 28 baada ya kusoma habari kumhusu na wamempatia matibabu kwa kipindi cha miezi miwili mpaka aliporuhusiwa Aprili 18 mwaka huu.

“Tusingemfahamu kama si Gazeti la Mwananchi kuandika habari zake, uongozi wa MOI tulipoona tunaweza kufanya hayo matibabu tulimchukua na kumtibu. Ni kweli Marwa hakuwa na uwezo kama ambavyo kitengo cha Ustawi wa Jamii waliona, hivyo tumemtibu kwa gharama za hospitali,” alisema Mvungi huku akisisitiza kuwa MOI isingependa kutaja gharama.

Matibabu aliyoyapokea Marwa ni ya kibingwa ambapo walianza kumsaifisha kidonda kilichokuwa kikivuja maji na usaha kichwani kwa miaka mingi na kumfanyia upasuaji wa awali wa kuondoa uchafu kichwani kabla ya upasuaji mkubwa wa kupandikiza fuvu jipya Machi 9.

“Ninajisikia vizuri sana siyo kama kipindi cha nyuma, kuna wakati mwingine huwa nasahau mambo fulani fulani, sikumbuki nilivyofanyiwa upasuaji ninachokumbuka kipindi cha nyuma hali yangu ilikuwa mbaya kwa sasa nina afadhali kubwa Mungu atasaidia nitapona kabisa.”

Ndivyo alivyoanza kuzungumza Marwa wakati wa mahojiano na Mwananchi akiwa nyumbani kwake Ukonga, Mombasa jijini Dar es Salaam.

Marwa anasema harufu iliyokuwepo huko nyumba haitoki, “Namshukuru Mungu kwa kuweza kunisaidia hata hili jambo limewezekana, nawashkuru wahudumu MOI walioweza kunisaidia msaada walionipatia ni mkubwa sana na kama wangeamua kunitoza gharama nisingeweza kufanikiwa matibabu nawaombe Mungu aweze kuwabariki.”

Hata hivyo Marwa anasema anaendelea kupona baada ya kuruhusiwa na sasa bado anapata maumivu katika mkono wake wa kushoto ambao uliathirika huko nyuma, “Nilipowaeleza madaktari wakaniambia ni hali ambayo itaisha na wataniangalia zaidi nitakapokuwa nikihudhuria kliniki.”


Ugumu wa maisha

Marwa anasema amepangiwa kuhudhuria kliniki kila baada ya wiki mbili, ameandikiwa dawa ambayo hata hivyo imekuwa changamoto kwake kuinunua kutokana kutokuwa na kipato, “Sijaweza kwenda kununua kwa kuwa sina fedha yoyote na waliniambia kwamba lazima nitumie hiyo dawa, hali yangu ya kiuchumi haijakaa vizuri.”

Marwa ambaye ni mkazi wa Tarime, Mara anasema kutokana na ugonjwa wake bado anatakiwa kuwa karibu na madaktari kwa kuhudhuria kliniki hivyo hawezi kurudi nyumbani kwao.

“Nawaomba Watanzania wenzangu waweze kunisaidia nifungue hata biashara yoyote ili niweze kutengeneza kipato nipate fedha za kutumia.”

Marwa aliwashukuru Watanzania waliomchangia awali, “Watanzania waliweza kunyoosha mkono wakanisaidia kiasi cha fedha ambacho kiliweza kutumika kwenye matibabu na fedha zingine mahitaji ya chakula wakati nipo hospitalini.”

Alisema kwa sasa amepanga nyumba lakini bado kuna changamoto anakabiliana nazo ikiwa ni mazingira kwani nyumba anayoishi haina miundombinu rafiki.

Mwananchi iliishuhudia nyumba hiyo inayoonekana haikumaliziwa ujenzi, “Nikitaka kuingia ndani ni shida na kama ikitokea nikakanyaga vibaya nikateleza ni shida kuingia, nyumba haina komeo la ndani wala la nje na mtu akifika akisukuma tu anaingia ndani.”

Licha ya changamoto alizozielezea Marwa bado nyumba hiyo haina vyoo vizuri kwani vilivyopo havisaidii mlango mwembamba hali inayompa changamoto anapohitaji kutumia maliwato.

Hata hivyo Marwa anasema licha ya kutamani kufanya kazi tena atakapopona ana nia ya kumrudishia Mungu fadhila alizomtendea.

“Mipango yangu ninataka kuja kufanya kazi ya Mungu, nilitamani nilipona kabisa nije nifanye kazi ya bwana kwa kuwa nintaendelea kuwa na imani na nimshkuru Mungu kwa msaada wake anaoendelea kunisaidia nami nitamfanyia kazi kwa uaminifu kabisa,” alisema Marwa.

Mke wa Marwa, Jane Marwa Ghati aliliambia Mwananchi kuwa anawaomba Watanzania wamsaidie kupata bima ya matibabu ili mume wake aweze kutibiwa mahali popote atakapokuwa.


Chanzo cha tatizo

Daktari bingwa wa upasuaji magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Hamis Shaban alizungumza na Mwananchi na kueleza chanzo cha tatizo la Marwa na matibabu sahihi ambayo mgonjwa huyo alipaswa kupewa

Anasema mgonjwa huyo alifika hospitalini wakati sahihi kwani hajakutwa na homa na ubongo wake haujaathirika isipokuwa kwa bahati mbaya alipata ugonjwa wa kifafa kutokana na kuchelewa matibabu.

Wakati Marwa akiwa amekaa miaka mitano pasipo uangalizi wa wataalamu wa afya, amepata madhara kadhaa ikiwemo kifafa, uono hafifu, kupooza sehemu ya mwili wake ikiwemo kupata ugonjwa wa kifafa.

Dk Shaban alisema maambukizi hayo yangeweza kumsababishia kupata degedege ambalo linaleta athari nyingine kama ulemavu, uwendawazimu, upofu, kutosikia, kulemaza mikono, miguu na mtindio wa ubongo,

Unaweza kumsaidia Marwa kwa kutumia namba 0747362904 iliyosajiliwa kwa jina Matinde Msyomi au piga simu kwa mhariri wa Mwananchi.