Ally Dangote auawa akiwatoroka polisi


Muktasari:

  • Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Salvas Makweli amesema Dangote aliuawa jana baada ya kupata jeraha la risasi wakati akiwatoroka polisi.

Arusha. Mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha leo wamejitokeza kushuhudia mwili wa kijana anayetambuliwa kwa jina la Ally Dangote (19) aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi, akidaiwa kutoroka baada ya kukamatwa.

 Dangote kabla ya kutajwa kuhusika na matukio ya mauaji alikuwa rumande Magereza kwa muda mrefu kwa tuhuma za mauaji na hatimaye mwaka huu aliachiwa huru na Mahakama kutokana na kukosekana ushahidi.

Akizungumzia kifo hicho leo Novemba 20, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Salvas Makweli amesema Dangote ameuawa baada ya kupata jeraha la risasi wakati akiwatoroka polisi.

"Ni kweli huyu mtuhumiwa alikuwa anasakwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za wizi na mauaji na leo baada ya kuwekewa mitego tulimkamata na wakati anakwenda kuwaonesha wenzake aliruka kwenye gari na ndipo alipigwa risasi na kutokana na kuvuja damu nyingi alifariki akiwa hospitali," amesema.

Amesema mtuhumiwa huyo amekuwa akiwakaba watu kuwapora simu, pikipiki na mali nyingine na wengine kuwajeruhi katika maeneo ya Unga Ltd, Esso na Daraja mbili.

"Katika operesheni iliyoendeshwa na polisi jamii wa mitaa mitatu kwa kushirikiana na wananchi maeneo ya Makaburi ya Banian, Kanisani na Tindiga ilifanikisha kumtia mbaroni Ally Dangote (19) mkazi wa Unga limited jijini hapa," amesema.

Katika Operesheni hiyo pia, polisi wamemkamata mtuhumiwa mwingine, Hashimu Kibwerezi (20) mkazi wa Osterbay jijini hapa na baada ya kuhojiwa alikiri kujihusisha na matukio ya uporaji na kuonesha baadhi ya mali walizokuwa wakipora ambazo zimekamatwa.

Akizungumzia tukio la kuuawa kwa Dangote, Mwenyekiti wa Kamati ya Polisi Jamii Mtaa wa kanisani, Abubakari Seif amesema kukamatwa kwa vibaka hao ni mafanikio makubwa kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbua.

"Hasa huyu Dangote amesumbua sana wananchi kwa kupora na wizi wa vitu vyao nyakati za mchana na usiku, leo kukamatwa na kufariki ni faraja kwa wakazi wa Arusha," alisema.

Mmoja wa wakazi wa Unga Ltd, David Frank alisema kwa mwezi mmoja walikuwa na hofu ya kijana huyo na kushindwa kutoka nyumbani usiku.

"Huyu kijana Dangote alikuwa hatari sana ameua zaidi ya watu watatu ikiwemo kumjeruhi mwanafunzi mmoja akitaka kumpora simu," amesema.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda Makweli amesema taarifa kamili ya tukio hilo itatolewa kesho.