Anayedaiwa kumuua mkewe, ajiua kwa kugonga treni

Muktasari:

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina na Omary amefariki leo Jumatano Juni 28, 2023 baada ya kujirusha kwenye treni eneo la Ubungo Maziwa kwa kudaiwa kumuua mke wake Mwanahamisi Mjeshi.

  

Dar es Saalam. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina na Omary amefariki leo Jumatano Juni 28, 2023 baada ya kujirusha kwenye treni eneo la Ubungo Maziwa kwa kudaiwa kumuua mke wake Mwanahamisi Mjeshi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinaeleza kuwa tukio hilo la mwanamke kuuawa limetokea leo asubuhi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Taarifa hizo ni za kweli na yeye amejirusha kwenye treni, lakini tunaendelea kufuatilia kwa karibu, taarifa zaidi nitazitoa,” amesema Muliro.

Akisimulia tukio hilo mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amesema wakati treni hiyo ikitokea Ubungo kuelekea Gerezani, ikiwa maeneo ya Maziwa mtu huyo akiwa na viatu mkononi alijitokeza gafla na kujirusha katika treni.

 “Tukio hilo la kujirusha limetokea saa 12 kasoro wakati treni ikitoka Ubungo kuelekea Gerezani, alijitokeza mwanaume akiwa anakimbia huku akiwa ameshika viatu mkononi na kujirusha kwenye treni,” ameeleza shuhuda huyo.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya watu kujiua na wengine kuua wenza wao sababu nyingi zikihusishwa wivu wa mapenzi na imani za kishirikina.