Anayedaiwa kupora Sh312.8 milioni Vodacom akosa dhamana
Muktasari:
- Mfanyabiashara, Godson Leonard (28) amefikishwa mahakamani kwa wizi wa zaidi ya Sh312.8 milioni mali ya Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Godson Leonard (28) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la wizi wa zaidi ya Sh312.8 milioni mali ya Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Leonard amefikishwa mahakamani hapo leo Mei 24,2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo alisomewa kosa hilo na Wakili wa Serikali, Tumaini Maingu.
Wakili Maingu akisoma hati ya mashtaka alidai kuwa kati ya Septemba Mosi na Novemba 30, 2021 eneo la Kigogo Freshi, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa huyo aliiba kiasi cha Sh312.8 milioni mali ya Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Mshitakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo alikana na upande wa Jamuhuri ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali.
Hakimu Shaidi alisema masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho pamoja na kitambulisho cha Taifa watakaosaini bondi ya Sh1 milioni kila mmoja.
Pia alisema kati yao mmoja awe na hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh20 milioni mbapo hati hiyo iwe imefanyiwa tathimini.
Hata hivyo, mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo alirudishwa rumande hadi Juni 6,2023 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.