Ardhi Yetu Programu ilivyobadili uelewa na kuleta manufaa kwa wananchi

Wanakijiji wa kijiji cha Olcholonyori kilichopo Simanjiro mkoani Manyara wakielekea kutafuta maji kwa kutumia usafiri wa Punda. Mabadiliko ya tabianchi yameleta athari kubwa kwenye maeneo hayo ikiwemo shida ya maji.
Muktasari:
- Wanajamii wa kijiji cha Kororngo kilichopo Simanjiro mkoani Manyara wakiwa kwenye moja ya mikutano ya kijiji hicho ambacho kimenufaika na Programu ya Ardhi Yetu.
Wanajamii wa kijiji cha Kororngo kilichopo Simanjiro mkoani Manyara wakiwa kwenye moja ya mikutano ya kijiji hicho ambacho kimenufaika na Programu ya Ardhi Yetu.
“Hakuna atakayeachwa nyuma” ni kaulimbiu ya wazi inayoweka msingi wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ikidhamiria kuleta matokeo chanya kwa watu wote.
SDGs ni mkusanyo wa malengo 17 yaliyopangiliwa kwa faida ya watu wote yaliyoanzishwa mwaka 2015 na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UN).
Kutokomeza umasikini wa aina zote kila mahali, njaa, kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora na kukuza kilimo endelevu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uwepo wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyotajwa kwenye malengo hayo.
Ili kuweza kufikiwa, uandaaji wake ulishirikisha wadau mbalimbali na kusisitiza haja ya kuweka mkakati wa utekelezaji na rasilimali za kutosha.
Mbali na utekelezaji wake, mafanikio ya malengo hayo yatapatikana ikiwa tu kutakuwa na ushiriki mkubwa wa wadau wote zikiwemo Serikali za inchi na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Tanzania ni moja ya mataifa yenye mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyojikita katika kuisaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.
CARE Tanzania ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali, lililosajiliwa chini ya sheria ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ya mwaka 2002 (Cap24) na iliyorekebishwa mwaka 2005.
Shirika la CARE limekuwa likitekeleza miradi yake kwa zaidi ya miaka 25 sasa tangu mwaka 1994 inayolenga kuziwezesha jamii kuondokana na umasikini uliokithiri na kuishi maisha yenye kuzingatia haki na usawa kwa wote. Walengwa wakuu wa shughuli za shirika la CARE Tanzania ni makundi maalum yasiyojiweza hasa wasichana na wanawake.
Programu ya Ardhi Yetu (AYP) ni miongo mwa jitihada muhimu zinazofanywa na shirika hilo ili kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii na kuhakikisha Taifa linafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu hususani namba 1, 2, 5, 13 na 15 ambayo yanaelekeza kutokomeza umasikini, njaa, kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora, kukuza kilimo endelevu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uwepo wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
CARE International Tanzania inatekeleza program ya Ardhi yetu kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Makamu wa Rais kitengo cha mazingira, idara mbalimbali na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kushughulikia haki za ardhi, mabadiliko ya tabianchi na kuweka mipango bora ya matumizi bora ya ardhi kwa jamii za wafugaji na wakulima.
Mashirika hayo ni; HAKIARDHI lililopo Dar es Salaam, Jumuiko la Maliasili Tanzania (Tanzania Natural Resource Forum, TNRF) lililopo Arusha na Shrika la Maendeleo la Jamii ya Wagufaji wa Parakuiyo (Parakuiyo Pastoralists Indigenous Community Development Organisation, PAICODEO) lililopo Morogoro.
Mei, 2018 HAKIARDHI, TNRF na PAICODEO chini ya ufadhili wa Shirika la CARE International Tanzania walianza utekelezaji wa program hii awamu ya pili baada ya kukamilika kwa wamu ya kwanza iliyotekelezwa mwa miaka minne kuanzia 2014 mpaka 2017 iliyokuwa imejikita katika kukabiliana na changamoto za ardhi.
Programu ya Ardhi Yetu awamu ya pili ni ya miaka minne kuanzia 2018 mpaka 2021 na inatekelezwa kwenye wilaya 11 za Tanzania Bara ambazo ni; Kiteto, Simanjiro, Chemba, Iringa Vijijini, Kilolo, Mufindi, Kilombero, Wilaya ya Morogoro, Morogoro vijijini, Mvomero na Kilosa.
Mbali na kushughulikia changamoto za ardhi, awamu hii ilijikita katia kutoa elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuisaidia jamii kutumia njia za kijadi na kisayansi kukabiliana na changamoto hiyo. Pia imejikita katika masuala ya usawa wa kijinsia, elimu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuzijengea jamii uwezo katika masuala ya ujasiriamali.
Katika program hii Shirika la CARE International limeweza kujenga uwezo wa mashirika ya HAKIARDHI, TNRF na PAICODEO jambo lilosaidia jamii za wafugaji na wakulima kupiga hatua katika kushughulikia haki za ardhi, mabadiliko ya tabianchi na kuweka mipango bora ya matumizi bora ya ardhi.
Programu hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa wakulima na wafugaji kwani kwa sasa jamii hizo zina uwezo wa kushughulikia haki zao za ardhi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kusimamia mipango bora ya matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro baina yao.
Mafanikio haya yalinifanya kusafiri kwenda Kisaki (Morogoro), kijiji cha Zambia, Kiteto, Manyara na vijiji vya Olcholonyori na Korongo vilivyopo Simanjiro Manyara.
Safari hii iliniwezesha kushuhudia mabadiliko makubwa ya uelewa na mitazamo ambayo wananchi wamepata kutokana na utekelezaji wa programu hiyo.
Kijiji cha Kisaki (Morogoro)
CARE International Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la HAKIARDHI wameifikia jamii ya wana Kisaki kupitia AYP II. Katika kijiji hicho washirika hao wamefanikiwa kutoa elimu kuhusu masuala ya ardhi ikiwemo sheria na haki za ardhi, haki za wanawake katika kumiliki ardhi na mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa HAKIARDHI, Cathbert Tomitho, kwa kutumia waangalizi wa ardhi (LRMs), AYP II imefanikiwa kutoa mafunzo ya masuala ya ardhi na mabadiliko ya tabianchi kwa wanajamii kwenye vijiji vya Lugalo, Ipilimo, Lukolongo, Ijia, Chita, Kisaki, Lundi na Mngazi.
Anasema waangalizi wa ardhi ni wananchi wa kawaida ambao wamepata mafunzo ya namna ya kusimamia masuala ya ardhi walioipata kutoka HAKIARDHI ili kutatua changamoto zinazoikabili jamii husika.
Pia, AYP II imefanikiwa kuanzisha maktaba za jamii za masuala ya Ardhi yenye machapisho yanayosaidia kutoa elimu na kuhamasisha usawa katika umilki wa Ardhi kati ya mwanaume na mwanamke kwenye maeneo ambayo mabaraza ya ardhi ya kata na wilaya hayawezi kufika.
“Tunajivunia kama taasisi kutokana na utekelezaji wa programu hii kwani kwa kiasi kikubwa imesaidia kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya haki za ardhi na mabadiliko ya tabianchi. Uelewa huu umewawezesha wananchi kufahamu haki za ardhi, kuzifahamu na kuzitatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kutambua haki za wanawake. Ushirikiano mzuri kati yetu na CARE International umesaidia kwa kiasi kikubwa kufikia mafanikio haya,” amesema Tomitho.
Mwangalizi wa ardhi kijiji cha Kisaki, Omary Kindamba amesema miaka 10 iliyopita Shirika la HAKIARDHI lilifika kijijini hapo ili kueleza shughuli wanazofanya likiwa na lengo la kupata wawakilishi watakaotoa usaidizi katika masuala ya utatuzi wa migogoro na haki za ardhi.
Amesema miaka kadhaa baadaye HAKIARDHI kwa kushirikiana na CARE International Tanzania walitoa mafunzo na semina mbalimbali kuhusu sheria za ardhi, utawala bora, utunzaji wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, utatuzi wa migogoro na haki za wanawake.
Amesema semina hizo zililenga jamii zilizoko pembezoni na zimesaidia kubadili mitazamo na kuongeza uelewa kwenye mambo mbalimbali.
“Kabla ya kupata semina hizi tulikuwa hatufahamu mambo mengi kuhusu masuala ya haki za ardhi. Mfano; kisheria kijiji kina mamlaka ya kutoa ardhi ya ekari 49 kushuka chini ikizidi hapo mamlaka hayo hiyo inahamia mamlaka ngazi ya juu,” amesema Kindamba.
Amesema ukosefu wa elimu ulisababisha wanakijiji kudhulumiwa ardhi yao kwa kigezo cha uwekezaji.
“Mfano; anakuja mtu kijijini anajiita mwekezaji na kutaka kupewa ardhi, kutokana na ahadi mbalimbali anazotoa wanakijiji wanashawishika na kutoa ardhi yao bila kufahamu madhara yatakayojitokeza baadaye wakiamini kwamba wakiihitaji wanaweza kuipata na ndiyo maana kila siku kuna migogoro ya wananchi na wawekezaji wakigombania ardhi,” amesema Kindamba.
“Wananchi wa Kisaki tunashukuru programu ya Ardhi yetu kupitia mashirika haya kwa kutufikia huku tuliko kutupa elimu hii, kwa kweli imetusaidia kwa sababu hivi sasa hatuwezi kudhulumiwa ardhi yetu kutokana na uelewa wa sheria na taratibu za ardhi tulioupata,” amesema Kindamba.
Amesema baada ya kupata elimu hiyo alianzisha darasa la masuala ya ardhi kwa ajili ya kuwafundisha wanakijiji wengine jambo ambalo limesaidia kusambaza elimu hiyo kwa wanajamii wengi kijijini hapo. Pia alifungua maktaba ya ardhi ambayo wanakijiji huitumia kusoma vitabu na vipeperushi vinavyohusu sheria na haki za ardhi.
“Baada ya kupata mafunzo haya niliamua kutoa elimu kwa wanakijiji wenzangu hivyo nilitumia vikundi mbalimbali, sehemu za michezo ili kuwafikia wengi na pia niliamua kufungua maktaba ya machapisho ya masuala ya ardhi nyumbani kwangu ili iwe rahisi kwa watu kujisomea vitabu na vipeperushi mbalimbali ambavyo HAKIARDHI na CARE International hunipatia nikihudhuria semina,” amesema Kindamba.
Moja ya wanafunzi walionufaika na darasa la ardhi kutoka kwa Kindamba, Lucas Lipewa amesema HAKIARDHI na CARE International imewasaidia kwa kuwapatia elimu hiyo kwani hivi sasa hawazulumiwi ardhi yao.
“Mimi ndiyo mwanafunzi wa kwanza kwenye darasa la ardhi chini ya Kindamba na nilivutiwa kujiunga na darasa hilo kwa sababu ni muhanga wa migogoro ya ardhi kutokana na kumpoteza kaka yangu aliyeuawa na watu kwa kugombani ardhi, hivyo darasa hili limekuja kunikomboa mimi na jamii yangu kwenye masuala ya ardhi,” amesema Lipewa.
“Kutokana na elimu niliyoipata nimefahamu haki zangu kama mwanamke na za wanawake wengine kwenye jamii yangu. Pia nimepata elimu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na sasa naweza kupigania haki zangu na za familia yangu,” amesema Ashura Mponda mkazi wa Kisaki.
Kijiji cha Zambia-Kiteto (Manyara)
CARE International Tanzania kwa kushirikiana na Shrika la Maendeleo la Jamii ya wafugaji wa Parakuiyo (Parakuiyo Pastoralists Indigenous Community Development Organisation, PAICODEO) wamefanikiwa kuvifikia vijiji kadhaa vilivyoko wilayani Kiteto mkoani Manyara kimojawapo kikiwa kijiji cha Zambia.
Kupitia AYP II washirika hao walifanikiwa kutoa elimu na mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi na kuwawezesha kupata taarifa za hali ya hewa ambapo taasisi ya PAICODEO kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wametoa elimu ya umuhimu wa taarifa za hali ya hewa katika masuala ya kilimo na ufugaji.
Mafunzo hayo yamewasaidia wananchi kubadili tabia kwa kuanza kuweka mipango mbalimbali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama kupanda mazao mchnganyiko, kutunza malisho kwa matumizi ya baadaye, kutumia taarifa za hali ya hewa za kimila na kisayansi katika misimu ya kilimo jambo lililowasaidia kuzuia kiasi cha mazazo kilichokuwa kinapotea awali kabla ya kupata mafunzo.
Ofisa Programu wa PAICODEO, Emmanuel Ole Kileli amesema shirika hilo lilianza kutekeleza AYP II mwaka 2018 kwenye wilaya nne za mikoa miwili ambayo ni; Morogoro (Mvomero, Kilosa na Morogoro Vijijini) na Kiteto Mkoa wa Manyara.
“Katika utekelezaji wa AYP II kwenye wilaya tajwa, PAICODEO tumefanya kazi na vikundi zaidi ya 30 vya kina mama ambapo vipo vya wakulima na wafugaji kwa kuwapa elimu kuhusu usimamizi wa ardhi, mabadiliko ya tabianchi, utunzaji wa maliasili na mazingira ambayo imewasaidia kutambua namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuanza kupanda mazazo mchanganyiko, kufahamu hali na viwango vya mvua na kuondoa changamoto ya migogoro ya ardhi,” amesema Ole Kileli.
Mwenyekiti wa Umoja wa Kinamama Kijiji cha Zambia (UMAZA), Kisio Kiteka amesema elimu waliyoipata kutoka kwa PAICODEO imesaidia kuwainua kiuchumi kwani wamefanikiwa kuanzisha vikundi vya kukopeshana pesa na kufanya miradi midogo midogo.
“Elimu tuliyopewa na PAICODEO kwa kushirikiana na CARE International imetusaidia kuanzisha kikundi cha UMAZA ambacho kinahusika na masuala ya ujasiriamali, kuweka na kukopa na matumizi bora ya rasilimali fedha,” amesema Kisio.
Amesema Umaza ilianzishwa mwaka 2018 baada ya kupata elimu kutoka PAICODEO kwa kuweka fedha Sh 1000 kwa wiki kila mwanachama, baada ya kupata kiasi fulani cha fedha wakaamua kutengeneza katiba na kukisajili kikundi hicho na baadaye wakafungua akaunti ya benki.
“Baada ya muda tulipata Sh 200,000 zilitokana na posho zetu tulizokusanya kutoka kwenye mafunzo ya PAICODEO ambazo zilitusaidia kuanzisha mradi wa kulima alizeti lakini kutokana na kuchelewa kupanda tulifanikiwa kuvuna gunia mbili pekee, baadaye tuliamua kuanzisha mradi mwengine wa kuchukua vitenge Dar es Salaam na kukopeshana, ambao ndiyo tunaendelea nao mpaka sasa. Kikundi hiki kimetusaidia katika maeneo mengi kama vile kukopeshana wenyewe kwa wenyewe, kuanzisha biashara na shughuli mbalimbali za kilimo,” anasema Kisio.
Akizungumzia namna walivyopewa elimu ya kukabiliana na migogoro ya ardhi kwa wakulima na wafugaji, Mjumbe wa Kamati ya migogoro kijiji hapo, Penina Emmanuel, amesema kabla ya ujio wa PAICODEO hali ilikuwa mbaya sana kwenye masuala ya migogoro ya ardhi.
“Huko nyuma hali ilikuwa mbaya, wakulima na wafugaji walikuwa wanapigana kila kukicha, jambo lililosababisha vifo na wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu lakini baada ya elimu tuliyoipata kutoka kwenye program hii suala la migogoro kwenye kijiji cha Zambia limekuwa historia,” amesema Penina.
Amesema hivi sasa wanaishi kwa amani katika kijiji hicho jambo ambalo limefanya shughuli za kiuchumi (ukulima na ufugaji) kufanyika bila wasiwasi na ikitokea changamoto ama mgogoro wowote wanaumaliza kwa njia ya mazungumzo bila kutumia nguvu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utabiri wa Kijadi waHali ya Hewa Zambia, Kombo Dengule amesema PAICODEO na CARE International kupitia AYP II wamewasidia kwa kiasi kikubwa kufahamu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutupa elimu ya utabiri wa hali ya hewa wa kisayansi na kuanzisha vikundi vya utabiri wa jadi.
“Elimu tuliyoipata kwenye kijiji chetu kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi imetusaidia katika shughuli zetu za kilimo kwa kiasi kikubwa. Zamani hatukuwa na uelewa kuhusu masuala kama vile mabadiliko ya kiwango cha mvua lakini PAICODEO walitupa semina kuhusu masuala ya hali ya hewa kwa kushirikiana na TMA, walituhamaisha kutumia utabiri wa jadi pamoja na kuchagua mazao ya kulima kutokana na hali ya hewa iliyopo,” amesema Dengule.
Amesema elimu hiyo imewahamasisha wanakijiji kufuatilia taarifa za hali ya hewa za TMA kupitia vyombo vya habari na utabiri wa jadi kutoka kwa wazee. Hali hiyo imewasaidia wakazi wa Zambia kuepuka kupoteza mazao kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Kororngo na Olcholonyori (Simanjiro) Manyara
Katika jitihada za kuwafikia Watanzania wengi, Care International kwa kushirikiana na Jumuiko la Maliasili Tanzania (Tanzania Natural Resource Forum, TNRF) waliifikisha AYP II wilayani Simanjiro kwenye vijiji vya Kororngo na Olcholonyori.
Vijiji hivyo ni miongoni mwa maeneo yanayokumbwa na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya wakulima na wafugaji, ukosefu wa huduma muhimu kama maji, hivyo kupitia programu hii wananchi wameelimishwa namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Mratibu wa AYP II kutoka TNRF, Rogath Massay amesema ushirikiano wao na CARE International kwenye utekelezaji wa program hiyo umeleta manufaa makubwa kwa wanajamii wa vijiji hivyo.
“TNRF tulipokea AYP II Mei 2018 na tukaanza kuitekeleza Julai 2018. Programu hii ilianza kwa semina iliyotolewa na CARE International iliyoshirikisha wadau mbalimbali ambapo pamoja na mambo mengine ilihusisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi, utabiri wa hali ya hewa, masuala ya ardhi, mazingira, migogoro ya wakulima na wagufaji, usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kiuchumi,” amesema Massay.
Amesema baada ya semina hiyo walianza utekelezaji wa programu ambapo walifanya utafiti kuhusu matumizi ya viashiria vya kiasili katika kutabiri mvua ukiwa na lengo la kufahamu namna ya kutumia viasharia hivyo na matokeo yake kwa manufaa ya jamii nzima jambo ambalo lilifanikiwa na sasa linawasaidia wanajamii kukabiliana na mabadiliko ya mvua kwa kutumia vikundi vilivyoanzishwa ambavyo vinafanya utabiri mara mbili kwa mwezi (tarehe 15 na 30).
Massay amesema pia, walifanya tafiti kuhusu masuala ya kijinsia ili kufahamu changamoto zinazowakabili wanajamii kwa lengo la kuwafahamisha wadau ikiwemo Serikali namna bora ya kuzitatua. Aidha, walitoa elimu ya kukabiliana na majanga mbalimbali, mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya ardhi na uanzishaji wa vikundi vya kijasiriamali.
Katibu wa Kikundi cha kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kijiji cha Olcholonyori, Yohana Mamasita amesema mafunzo waliyopata kutoka kwenye programu hiyo yamebadilisha kabisa namna ambavyo walikuwa wanaishi hapo zamani.
“Tumepata elimu kuhusu kukabiliana na majanga yanayojitokeza katika jamii kama vile njaa, mafuriko na mabadiliko ya tabianchi kwani awali tulikuwa tunalima kilimo cha mazoea ambacho wakati mwengine tulikuwa tunakosa mavuno kabisa, hivyo program hii imeleta mabadiliko ya chanya kwetu,” amesema Mamasita.
Mwanakijiji wa kijiji cha Korongo, Edina Lazaro amesema TNRF na Care International wamewasaidia kufahamu haki za wanawake katika jamii kutokana na elimu ya masuala ya jinsia waliyowapatia.
Changamoto
Kila penye mafanikio hapakosi changamoto. Utekelezaji wa programu hii umeonyesha kuwa bado kuna uhitjai mkubwa wa jamii kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi, usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi.
Vijiji vilivyopo pembezoni bado vinakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kama maji safi na upatikanaji wa taarifa sahihi za mabadiliko ya hali ya hewa. Programu ilijiktia zaidi katika kutoa mafunzo na kujenga uwezo, hivyo upo uhitaji wa jamii kuwezeshwa kifedha na vitendea kazi ili waweze kutumia vyema elimu waliyoipata.
Kwa taarifa zaizdi
Tafadhali wasiliana na;
CARE Tanzania
Barabara ya Ruhinde, Kitalu namba # 175B
Ada Estate Kinondoni Upper
S.L.P 10242, Dar es Salaam
Simu: +255 -22-2668048, +255 -22-2668061
Baruapepe: [email protected]