Askofu Bagonza ataka jamii kuacha chuki, iwe na upendo

Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza (wapili kulia) akimkabidhi kitabu Clement Nsherenguzi katika hafla fupi ya uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika wilayani Karagwe

Muktasari:

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza ameitaka jamii kuwa na upendo, amani na kuacha chuki akidai kufanya hivyo wataongeza miaka ya kuishi duniani.

Karagwe. Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Benson Bagonza ameitaka jamii kuwa na upendo, amani na kuacha chuki akidai kufanya hivyo wataongeza miaka ya kuishi duniani.

Dk Bagonza ameyasema hayo Oktoba 31, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Clement Nsherenguzi (87) mkazi wa Kata ya Bugene Wilaya ya Karagwe.

"Nsherenguzi alikuwa na upendo; kuna siku alikuwa na mgogoro na mtu nikawasuruhisha yule mtu akataka kumpiga huyu mzee lakini yeye alinyenyekea na kuomba msamaha ili yaishe, hakutaka kuwa na chuki na mtu na hiyo imemsaidia akaweza kufikia umri alio nao, hata na sisi tumuige ili tuishi miaka mingi duniani"amesema Dk Bagonza

Katika hatua nyingine, Dk Bagonza amewashauri Watanzania kuandika historia zao wakiwa hai badala ya kusubiri kuandikwa na watu wengine pindi wanapofariki dunia akidai wanapoandika wenyewe wanajua kipi waandike na kipi waache.

Ametolea mfano wa aliyekuwa Katibu Muhutasi wa Baba  wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere, marehemu Joan Wicken akisema kabla ya kifo chake alipanga kuandika historia ya Hayati Mwalimu Nyerere kwa kutumia kumbukumbu mbalimbali zilizokuwa zinahifadhiwa (dayaries) lakini akasita na kusema historia hiyo itaandikwa baada ya miaka 30.

"Maisha ni kitabu lakini kuna vitu vya kuandika na kuna vitu haviandikiki, nilipewa mwaliko kwenda mjini London kuzindua kitabu cha hayati baba wa Taifa sikwenda lakini kitabu hicho kilizinduliwa siku ya Nyerere day Oktoba 14, 3023.

“Kitabu hicho kilipangwa kuandikwa na aliyekuwa katibu muhtasi wake kutokana na kumbukumbu mbalimbali za hayati Julius  Kambarage Nyerere lakini alisita na kusema kiandikwe baada ya miaka 30 hiyo ina maana yake, ili wawepo wazee baadhi wanaomjua baba wa Taifa" amesema Askofu Bagonza

Akizungumzia kitabu chake kilichochapishwa 2023 na Tanzania Educational Publishers Ltd (TEP), Nsherenguzi aliyekuwa Mwenyekiti wa Shirika la Saidia Wazee Karagwe (Sawaka) amesema lengo la kuzindua kitabu hicho chenye sura 19 na kurasa  163 ni kuweka kumbukumbu za maisha yake na vitu alivyofanya kwa faida ya jamii na kizazi chake.

Rafiki wa Nsherenguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TEP, Pius Ngeze amesema wazo la kuandika kitabu hicho lilitolewa na Hope binti wa Nsherenguzi na kukubaliwa kisha mzee huyo alianza kuandika na hatimaye kitabu hicho kuzinduliwa jana.