Mbowe, Askofu Bagonza kuongoza mapokezi ya Lema KIA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akizungumza jambo na Askofu Dk Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) jimbo la Karagwe. Picha na mtandao
Muktasari:
- Lema anatarajiwa kutua nchini Machi Mosi tangu alipondoka Novemba 2020 na familia yake kuelekea Nairobi nchini Kenya na baadaye kuelekea nchini Canada, akidai kutishiwa maisha yake.
Arusha. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajia kuongoza mapokezi na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Godbless Lema, Machi Mosi mwaka huu, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akiwa na viongozi kadhaa wa dini.
Lema aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kuanzia mwaka 2010 hadi 2020, alikimbilia nchini Canada kupitia Nairobi nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa 2020 akiwa na familia yake kwa madai ya kutishiwa maisha yao.
Wengine wanaotarajia kushiriki katika mapokezi hayo ni pamoja marafiki wa Lema, Askofu Dk Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) jimbo la Karagwe na Sheikh Rajabu Katimba na Askofu wa Kanisa la Uamsho la Morovian, Emmaus Mwamakula.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 23 kwa simu, Lema amesema anawashukuru viongozi hao wa dini, kumuahidi kuja kumpokea anaporejea.
"Taratibu zote na kurejea nchini, zinaendelea vizuri na Mungu akipenda Machi mosi ntarejea nchini ambapo pamoja na mambo mengine tutakuwa na mikutano kadhaa barabarani na baadaye uwanja wa Relini jijini Arusha," alisema
Lema alisema anarejea nchini kuendeleza siasa na demokrasia na kuna mengi amejifunza akiwa nchini Canada ambayo anatarajia kuwa yatasaidia maendeleo ya jimbo la Arusha na Taifa kwa ujumla.
"Kuna kampuni nikifika natarajia kuizindua ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa ikitoa ufadhili wa masomo na kubadilishana uzoefu," amesema.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Lema, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa amesema maandalizi yote muhimu ya mapokezi ya Lema yamekamilika.
"Tumejipanga vizuri na tunawaalika wakazi wa Arusha, Kilimanjaro na maeneo jirani kujitokeza kuanzia uwanja wa KIA hadi Arusha mjini, katika mapokezi wa Kamanda Lema," amesema
Alisema Lema licha ya kufanya mikutano kadhaa akiwasili nchini, pia anatarajiwa kuongoza vikao vya Chadema kanda hiyo kwa kuwa ndiye mwenyekiti.
Lema pamoja na viongozi kadhaa, akiwepo Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu wameanza kurejea nchini kufuatia mazungumzo ya maridhiano yanayoendelea kati ya chama hicho na CCM na Serikali.