Sababu tano Wajackoyah, kumpokea Lema nchini

Aliyekuwa mgombea urais Kenya mwaka jana, George Wajackoyah (kushoto) akizungumza  na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema (kulia).

Moshi/Arusha. Aliyekuwa mgombea urais Kenya mwaka jana, George Wajackoyah kutoka chama ya Root, ni miongoni mwa wanasiasa watakaompokea mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema anayetarajia kurudi nchini Machi mosi mwaka huu akitokea nchini Canada.

Lema alikimbilia nchini Canada Novemba mwaka 2020, baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu kwa kile alichodai kunusuru maisha yake baada ya kupata taarifa anataka kuuawa.

Mwanasiasa huyo ameliambia Mwananchi, kuwa anarejea nchini kuendeleza demokrasia hasa baada ya kuona mazingira ya sasa chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ni tofauti na yaliyomfanya akimbie nchini.

Maandalizi ya kumpokea Lema yamezidi kushika kasi huku kiu ya baadhi ya watu ni kutaka kujua sababu za Wajackoyah kushiriki kwenye mapokea hayo na baadaye kuhutumia mkutano wa hadhara ambao pia Lema atahutubia.

Wajackoyah kupitia Chama cha Roots of Kenya, alichuana na William Ruto wa United Democratic Alliance (UDA), Raila Odinga wa Azimio la Umoja Kenya One na Mwaure Waihiga wa Agano Party, ambapo huku Ruto aliibuka mshindi, akifuatiwa na Odinga huku Wajackoyah akishika nafasi ya tatu.

Miongoni mwa sababu Wajackoyah kushiriki mapokezi ya Lema ni uhusiano wa kifamilia na kirafiki walionao wawili hao.

Sababu nyingine ni kufanikisha (Lema) pamoja na familia yake kukimbilia nchini Kenya wakitumia gari ya mwanasiasa huyo wa Kenya.

Wajackoyah ambaye ni mwanasheria wa kimataifa, ndiye aliyemnusuru Lema asirejeshwe nchini baada ya Serikali ya Kenya kutaka kufanya hivyo kwa kile kilichodaiwa kukwepa kuingia kwenye mvutano na Tanzania. Mgombea urais huyo, alifungua kesi Mahakamani kuzuia Serikali ya Kenya iliyokuwa chini ya Rais Uhuru Kenyatta isimrejeshe Lema hapa nchini.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Lema alisema Wajackoyah na rafiki zake wengine ndiyo waliofanikisha aishi jijini Nairobi kwa takriban wiki tatu na baadaye kwenda nchini Canada.

Lema alisema bila ya mwanasiasa huyo wa Kenya aliyejizolea umaarufu mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, pengine leo hii asingekuwa hai kwa kuwa alipokamatwa alipewa tuhuma za kutaka kuiangusha Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikiongozwa na John Magufuli.

Katika mazungumzo yake Lema alisema Wajackoyah, ndiye aliyekuwa akizungumza na viongozi mbalimbali ndani na nje ya Kenya kuwaeleza kuwa Lema si mhaini bali anakimbia nchi kunusuru maisha yake kutokana na masuala ya kisiasa.

“Tuna urafiki wa siku nyingi na Wajackoyah, huyu jamaa kanisaidia sana na ajua sheria za kimataifa ndiyo maana nimeona ni muhimu akawepo siku nitakayorejea Tanzania na ahutubie wananchi kuwaeleza hali ilivyokuwa” alisema

Lema alisema kuwa wakati wote akiwa nchini Kenya, Wajackoyah alikuwa akiendelea kuwasiliana na watu mbalimbali kuhakikisha anakwenda katika nchi salama pamoja na kuepusha msuguano kati ya Tanzania na Kenya.

“Suala langu lilikuwa linakwenda vibaya kwa kuwa ilionekana Serikali ya Kenya inalinda wakati natuhumiwa lakini kwa kuwa Wajackoyah alikuwapo na anazijua sheria ilikuwa ngumu mimi kurudishwa nchini tena baada ya mahakama kuzuia jambo hilo na mpaka nilipoondoka hakukuwa na tatizo” alisema

Lema, alisema kwa kuwa Wajackoyah alimsaidia kisheria anataka aje aone shughuli za kisiasa nchini zinavyokwenda baada ya kifo cha John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021


Mapokezi yake

Katika maandalizi ya kumpokea Lema kutoka Canada, licha ya wilaya na mikoa jirani kushiriki, Jiji la Arusha lenye kata 25, limejipanga kuwa na mabasi manne aina ya Toyota Coaster na Toyota Hiace nne za binafsi na kufanya magari kuwa zaidi ya 150.

Lema ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi viwili kuanzia mwaka 2010 hadi 2020.

Kada huyo, ni miongoni mwa makada wa chama hicho walioikimbia nchi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 wakihofia usalama wao akiwamo Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ambaye amesharejea nchini.

Hii ni baada ya kubadilika kwa utawala na kuingia kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alitoa hakikisho la usalama na hiyo ndio iliyomsukuma Lissu kurejea nchini Januari 25, 2023.

Lissu aliishi uhamishoni nchini Ubelgiji tangu mwaka 2018 alipokwenda kwa matibabu akitokea Kenya, baada ya kunusurika katika jaribio la kumuua, lililofanywa na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 jijini Dodoma.

Hata hivyo, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Lissu alirejea nchini na kupitishwa na Chadema kugombea nafasi ya urais, lakini baada ya uchaguzi huo, aliikimbia nchi kwa kile kilichoelezwa ni kuhofia usalama wake.


Mapokezi ya Lema yatakavyokuwa

Akizungumza na Mwanachi, Mratibu mkuu wa maandalizi ya mapokezi hayo, Amani Golugwa alisema Lema anatarajiwa kuwasili nchini Machi Mosi mwaka huu saa sita mchana kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) . Tayari Jiji la Arusha limeanza kuwa na harakati mbalimbali kuelekea siku ya kurejea kwa Lema, gari la matangazo limekuwa likipita mitaani na kupiga nyimbo za kumkaribisha nyumbani mwanasiasa huyo.

“Tumeanza kikao cha kwanza jana (juzi) kwa viongozi wa kata zote za Jimbo la Arusha Mjini na tumeunda kamati kushughulikia mapokezi na tumepeana maelekezo yatakayowaongoza viongozi kutekeleza hili,” alisema.

Alisema mapokezi hayo yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nje akiwamo Wajackoyah na viongozi wa kitaifa, wajumbe wa kamati kuu ya Chadema, wabunge wa zamani, viongozi, wanachama na wananchi.

Viongozi wa Chadema ambao tayari wamethibitisha kushiriki mapokezi hayo na baadaye katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Jijini Arusha ni Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, mchungaji Peter Msingwa na Ezekia Wenje.

“Siku hiyo ya Machi Mosi tutakutana Kia saa tano na nusu (asubuhi) kusubiri ndege itakayokuwa na mwenyekiti wetu wa kanda ya kaskazini na saa sita na nusu mchana na tutaanza safari ya kuelekea Arusha mjini,” alisema Golugwa. Akiwa njiani, atazindua tawi la chama hicho eneo la Tengeru kabla ya kunguruma katika mkutano mkubwa wa chama katika viwanja vya relini Arusha, mkutano ambao harakati za maandalizi yake zimeanza kuonekana.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema mapokezi ya Lema yatakuwa makubwa na kwamba viongozi na wananchi kutoka majimbo na wilaya zote watashiriki.


Balozi Njolay, wananchi wafunguka

Akizungumzia ujio wa Lema, mwanasiasa mkongwe nchini na aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa mikoa tofauti kabla ya kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Daniel Ole Njoolay, alisema ujio wake unatia hamasa ya maendeleo.

Hata hivyo, Balozi Njolay alitahadharisha kuwa wanasiasa hao watumie vyema majukwaa hayo kujenga hoja zenye mashiko kwa maendeleo ya nchi akisisitiza kuwa ruksa hiyo ya mikutano isitumike kama vita ya kushambuliana.

Akizungumzia ujio wa Lema, mmoja wa wakazi wa Jijini Arusha, Theresia Mitawas alisema kuwa hali hiyo inaleta tafsiri nzuri ya kisiasa machoni mwa Watanzania na kuichangamsha tofauti na ilivyokuwa imedumaa.