Askofu Gwajima ahojiwa akiwa amesimama Kamati ya Bunge

Askofu Gwajima ahojiwa akiwa amesimama Kamati ya Bunge

Muktasari:

  • Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima amekataa kuketi katika Kikao cha Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na badala yake alitaka kusimama kwenye kipindi chote cha uendeshaji wa shauri hilo.


Dodoma. Mbunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima amekataa kukaa kwenye kiti  katika Kikao cha Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na badala yake alitaka kusimama kwenye kipindi chote cha uendeshaji wa shauri hilo.

Gwajima alihojiwa kwa mara ya kwanza na kamati hiyo Agosti 23, 2021 ambapo mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka amesema kuwa mahojiano bado yanaendelea.

Leo Jumatano Agosti 25, 2021, ni mara ya pili kufika katika kamati hiyo baada ya mara ya kwanza shauri hilo kutomalizika.

Hata hivyo  baada ya kuwasili katika ukumbi huo na kukaribishwa kiti, Gwajima alikataa kukaa na kusema akisimama atakuwa ‘comfortable’ zaidi.

“Hakuna shida leo nitasimama nishazoea kusimama,”amejibu Gwajima baada ya kutakiwa kuketi katika kiti.

Jambo hilo lilimfanya Mwakasaka kumuuliza mara kadhaa Gwajima kama anasababu maalum inayomfanya asikae kwenye kiti lakini mbunge huyo alijibu kuwa amezoea kusimama.

Alipoulizwa na Mwenyekiti kama atatumia kipaza sauti kilichoandaliwa, Gwajima alijibu kuwa hana shida kutumia kipaza sauti hicho.