Askofu Gwajima, Silaa waondolewa ujumbe Kamati ya Bunge

Muktasari:

  •  Wabunge Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga) ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge wameondolewa kwenye kamati hiyo hadi itakapoamuliwa vinginevyo.



Dodoma. Wabunge Josephat Gwajima (Kawe) na Jerry Silaa (Ukonga) ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge wameondolewa kwenye kamati hiyo hadi itakapoamuliwa vinginevyo.

Wabunge hao wameitwa mbele ya kamati hiyo wakituhumiwa kusema uongo, kushusha hadhi na heshima ya Bunge.

Gwajima alianza kuhojiwa jana na kamati hiyo kwa zaidi ya saa mbili na kesho ataendelea kuhojiwa, huku Silaa naye atahojiwa leo mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Emmanuel Mwakasaka.

Kwa mujibu wa Mwakasaka, kamati hiyo ina jumla ya wajumbe 24 wakiwamo Gwajima na Silaa na sasa imebaki na wajumbe 22.

“Unapotuhumiwa mara nyingi, wewe ndio mshtakiwa zipo taratibu zinafuata. Kama wewe ni mtuhumiwa huwezi kuwa hakimu kwenye kesi yako mwenyewe,” alisema.

Alipoulizwa ni lini waliondoka katika ujumbe wa kamati hiyo, Mwakasaka alisema: “Ninapozungumza na ninyi hawa (Silaa na Gwajima) si wajumbe wa kamati hii.”

Kuhusu kama wanaweza kurejeshwa kwenye kamati, mwenyekiti huyo alisema wanaweza iwapo Spika (Job Ndugai) atataka kufanya hivyo kwa sababu ndiye anayeteua wajumbe wa kamati.

Hata hivyo, alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa kina kwa sababu mwenye mamlaka ya kuwarejesha ni Spika wa Bunge kwa kuwa liko ndani ya madaraka yake.

Jumamosi wiki iliyopita Spika Ndugai aliamuru Gwajima na Silaa wapelekwe kwenye kamati hiyo, ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Gwajima alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo jana wakati Silaa atatakiwa kufika kwenye kamati hiyo leo saa 7.00 mchana.