Askofu Malasusa: Walimu wasio na maadili hawafai

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Askofu Alex Malasusa.

Muktasari:

  • Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Askofu Alex Malasusa amesema walimu wasio na maadili hawafai ikiwa ni katika kupinga mmomonyoko wa maadili kwa walimu ambao ndio walezi wa watoto.

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Askofu Alex Malasusa amesema walimu wasio na maadili hawafai huku akiwataka kuwa walezi bora kwa wanafunzi.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Elimu ya Dayosisi hiyo ikiwa inaadhimisha miaka 30 ya elimu leo Machi 18, 2023 Kibaha mkoani Pwani, Askofu Malasusa amesema walimu wasio na maadili katika shule za kanisa hawafai.

“Tunapohisi mwalimu anahisiwa katika mambo ambayo hata masikio yanawasha kuyasikia huyo hafai katika shule za kanisa, tuweke utaratibu ambao mwanafunzi ataweza kutoa taarifa juu ya kila mwalimu,” amesema Askofu Malasusa.

Amesema ni wakati kwa kanisa kufanya utafiti juu ya kila mwalimu ili kufahamu uwezo wake na kuona kama anaweza kuleta matokeo chanya.

Pia Askofu Malasusa amewataka walimu kuwa walezi kwanza kwani katika kuwa mlezi ndio matokeo chanya yatakapo patikana.

Askofu Malasusa amesema shule za makanisa siyo shule binafsi bali ni shule zinazoendeshwa kiroho kwani shule hizo hazisubiri kupata fedha kutoka kwenye shule hizo kwa sababu kuna watu ambao hawana uwezo.

“Ninaomba shule hizi zifahamike hasa kwa serikali kwamba shule hizi sio binafsi bali ni shule za kiroho,” amesema Askofu Malasusa.

Akielezea tofauti kati ya shule binafsi na shule za kiroho amesema katika shule binafsi ni rahisi kukuta shule ya msingi wanafunzi wanalipa ada milioni 9 lakini hakuna shule ya kiroho ambayo wanalipa kiasi hicho cha fedha.

Aidha Askofu Malasusa amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano ambao limekuwa likiuonyesha hasa katika kipindi cha majanga ya moto katika shule zinazomilikiwa na dayosisi hiyo.

“Tunajisikia vizuri kuwa raia wa Tanzania na kuona kuwa kumbe zile kodi tunazolipa zinafanya kazi vizuri, muendelee vizuri japo sina hakika kwamba mikoa mingine wanapata ushirikiano kama tunaopata Mkoa wa Pwani, tuna kila sababu ya kutoa shukrani sana,” ameongeza Askofu Malasusa.

Askofu Malasusa pia amezishukuru sharika mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitolea misaada mbalimbali katika kipindi chote cha miaka 30 katika kufanikisha elimu kwa kukubali kuchangia mfuko maalumu ambao ulianzishwa kwa ajili ya elimu.

“Kama tulivyosikia mfuko huu tayari umeanza kutoa ufadhili (Scholarship) kwa asilimia 100 kwa wale wasiojiweza, lakini pia tuangalie namna ya kufanya ili kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri,” amesema.

Akisoma risala maalumu kwa ajili ya siku hiyo kanisani hapo, kiongozi wa dawati la elimu katika dayosisi hiyo, Agness Lema amesema mpaka sasa Dayosisi hiyo inamiliki chuo kikuu kimoja, chuo cha elimu kimoja, seminari moja, shule za sekondari mbili, shule mbili za msingi na shule za awali 49.

Aidha Agness ameitaka serikali kutoa msaada wa vifaa vya kufundishia katika shule za dayosisi hiyo ikiwemo vitabu vya ziada na kiada.

Akizungumzia suala la wazazi kuwashirikisha watoto wao katika migogoro ya kifamilia na kupelekea kuwaathiri kisaikolojia Agness amesema “rai yetu kwa wazazi, wasiwashirikishe watoto katika magomvi yao ili kuepuka kuwaathiri watoto kisaikolojia,” amesema.