Askofu Shoo alia na ulevi vijana Kilimanjaro

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo.

Muktasari:

  • Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) anayemaliza muda wake, Askofu Fredrick Shoo, amesema tatizo la ulevi kwa vijana limekuwa kubwa mkoani Kilimanjaro, akiitaka jamii kushirikiana na Serikali na kanisa kukemea tatizo hilo.

Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) anayemaliza muda wake, Askofu Fredrick Shoo, amesema tatizo la ulevi kwa vijana limekuwa kubwa mkoani Kilimanjaro, akiitaka jamii kushirikiana na Serikali na kanisa kukemea tatizo hilo kunusuru nguvu kazi ya Taifa.

Dk Shoo, ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, ametoa rai hiyo leo Desemba 27, 2023, wakati akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa wana Dayosisi hiyo waishio safarini.

Mkutano huo umefanyika uhuru Hoteli mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ukishirikisha zaidi ya wajumbe 444.

"Ukosefu wa ajira kwa vijana wetu bado ni tatizo kubwa sana kwa Mkoa wetu wa Kilimanjaro. Sehemu kubwa ya vijana wetu wamejiingiza katika ulevi na hata kuvuta bangi na dawa nyingine za kulevya.

"Tusipojitahidi kuondoa tatizo hili, hata sisi tulio wazima tutaathirika kwa namna mbalimbali ikiwemo usalama wa familia zetu na mali tulizonazo huku nyumbani,” amesema.

Akizungumza suala hilo katika mkutano huo, Mkuu wa mkoa mstaafu, Agrey Mwanri amesema zinahitajika jitihada za pamoja za Kanisa, serikali na jamii katika kumaliza tatizo hilo la ulevi.

"Ukiona mtu anapiga maji, maana yake anadhoofisha uwezo wake wa kufikiri na vitu hivyo vinafanywa na watu ambao hawana kazi ya kufanya. “Kanisa lina kazi ya kulea na kutunza, kanisa lina kazi ya kulinda imani na jambo hili ni letu sote, tushirikiane na viongozi wa serikali na kanisa ili kulitokomeza, kwani linatishia nguvu kazi ambayo ni vijana,” amesema.

Uchaguzi

Katika hatua nyingine, Dk Shoo amewataka waumini wa kanisa hilo wenye sifa za uongozi, kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika mwakani 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

Dk Shoo, amesema Dayosisi hiyo imeweka mpango mkakati wa miaka mitano 2024-2028, wenye vipaumbele vitano ikiwemo haki za kimazingira, kiuchumi, kijamii na kisiasa ambapo watashiriki shughuli za kiserikali, hasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu.

"Pia kushiriki shughuli za kiserikali hasa tukijua kwamba mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 kutakuwepo na uchaguzi mkuu.

"Ninaomba sana wana dayosisi yetu popote mlipo na mtakapokuwa muweze kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima na kwa wale ambao wanaona wana vipawa waweze kugombea nafasi kuanzia ngazi za vijiji na sisi tukiona wale wanaofaa tuwasukume ili wagombee,” amesema.