Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Shoo atoa msimamo mgogoro Konde

Muktasari:

  • Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesema lazima uamuzi wa uongozi uheshimiwe na kuwashutumu maaskofu watatu anaodai wanapotosha kuhusu mgogoro uliopo katika Dayosisi ya Konde.

  

Moshi/Mbeya. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesema lazima uamuzi wa uongozi uheshimiwe na kuwashutumu maaskofu watatu anaodai wanapotosha kuhusu mgogoro uliopo katika Dayosisi ya Konde.

Askofu Shoo amesisitiza kuwa mkutano uliomng’oa aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo, Dk Edward Mwaikali ulikuwa halali na kufafanua kwamba uongozi wake na muda wa halmashauri uilikuwa umemalizika tangu mwaka 2021.

“Wana Konde wanasema amani imerejea kwa asilimia 98. Wanasema wao ndio waliochagua viongozi. Mimi nasema viongozi wapya watabarikiwa tu, tutamweka wakfu askofu mpya na kuwaingiza viongozi wapya kazini,” alisema.

Askofu Shoo ambaye ni mkuu wa dayosisi ya kaskazini, alitoa kauli hiyo jana katika Usharika wa KKKT Moshi mjini baada ya kumaliza mahubiri ya Pasaka ikiwa ni mara ya kwanza tangu ulipofanyika mkutano uliomwondoa madarakani Dk Mwaikali.

Kiongozi huyo, alitumia nafasi hiyo kufichua kiini cha mgogoro wa Konde kuwa ni Dk Mwaikali na halmashauri yake kuhamisha makao makuu bila kupata baraka za mkutano mkuu wa wana Konde.

Katika mkutano uliomng’oa Askofu Mwaikali na kuiondoa halmashauri yake, alisema wao walikuwa waangalizi tu. Tayari Dk Mwaikali amefungua kesi mahakamani kupinga kuvuliwa wadhfa wake katika Mahakama Kuu kanda ya Mbeya akilishtaki Baraza la Wadhamini KKKT na watu wengine 28 akiwamo Askofu Shoo.

Jana, Askofu Shoo aligusia kesi hiyo akisema “tumeambiwa tumepelekwa mahakamani na askofu aliyemaliza muda wake, akidi ya mkutano uliomng’oa ilitimia. Mbona watumishi wa Mungu tumefika mahali ambapo hata tunapokosea hatutaki tuambiwe baba askofu, mchungaji, wewe mtumishi hapa hujaenda sawa, ukiambiwa hivyo unakasirika, unataka kupigana vita.”

Alisema jambo hilo linaliumiza kanisa kiini kikiwa viongozi kusahau wajibu wao. Mbele ya waumini wao makao makuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Shoo alisema kipo kikundi kidogo cha watu kilichoamua kulichafua kanisa kupitia vyombo vya habari.

“Ukisoma kwa makini utalijua tu kwamba ni habari za kikundi kidogo bahati mbaya sana kuna Shoo bila kuwataja.

Kuhusu mgogoro huo, alitetea uamuzi wa kumwondoa Askofu Mwaikali akisema mkutano wa Machi 22 ulikuwa halali na kabla ya kufanyika, Dk Mwaikali ambaye alikuwa amemaliza muda wake alisaini makubaliano kwamba mkutano mkuu ufanyike na aliridhia kuundwa kwa kamati ya mkutano huo.

“Wamechagua askofu mpya, wamechagua msaidizi wa askofu mpya na halmashari kuu mpya na ni mkutano halali uliokuwa na akidi,” alisema Askofu Shoo.

Waumini KKKT mbaroni

Wakati hali ikiwa hivyo, jana Jeshi la Polisi lililazimika kuwakamata waumini wa KKKT Dayosisi ya Konde Usharika wa Mbalizi waliokuwa wakizuia mchungaji wa usharika huo, Atupele Mlawa kuingia kanisani hapo.

Taarifa zilieleza kuwa baadhi ya waumini wamekuwa wakimtuhumu mchungaji huyo kwa matumizi mabaya ya mali za kanisa.

Hata hivyo, kundi jingine la waumini liliingilia kati likishinikiza mchungaji huyo kuingia kanisani kuendesha ibada hali iliyosababisha polisi kufika kanisani hapo na kuwakamata baadhi ya viongozi kwa mahojiano hivyo ibada kutofanyika.

Mwandishi wetu aliwakuta waumini wakiwa katika makundi huku baadhi wakilaani hatua ya kufukuzwa kwa mchungaji huyo na wengine wakisisitiza ili amani iwepo lazima Mlawa aondoke.

Mmoja wa waumini hao aliyejitambulisha kwa jina la Jacob Mwaisango alisema walishampa barua ya kuondoka lakini walishangaa kumwona akiingia kanisani hapo kutaka kuendesha ibada kinyume na taratibu.

Akizungumzia sakata hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei alisema hawataki kuona uvunjifu wa amani katika maeneo yoyote ya jamii.

“Baada ya kupata taarifa niliagiza askari waende eneo la tukio, viongozi waliokamatwa wamepewa maelekezo ya nini cha kufanya kwa sababu huo mgogoro tulishaelekeza waupeleke mahakamani ili mwenye haki apewe,” alisema Matei.

Viongozi wanaodaiwa kuchukuliwa na polisi kwa mahojiano ni Mchungaji Mlawa na msaidizi wake, Lusajo Sanga na Mkuu wa Jimbo la Mbeya Magharibi, Judith Kajela.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Saddam Sadiki.