ATCL yaongeza ushindani anga la Afrika Mashariki

Friday November 26 2021
New Content Item (1)
By Ephrahim Bahemu

Dar es Salaam. Baada ya miaka 15 ya bila safari Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) limerejesha safari zake kati ya Dar es Salaam na Nairobi safari ambayo inatajwa kuwa itaongeza ushindani wa kibiashara katika anga la Afrika Mashariki husuani baina ya majiji hayo makubwa.

ATCL itakuwa ikifanya safari mbili kwa siku moja asubuhi na nyingine jioni kwa kutumia Ndege aina ya Airbus A220-300 yenye uwezo wa kupakia abiria 132 kati yake 12 zikiwa za daraja la juu (Business Class).

Kwa kuanzisha safari hiyo hivi sasa mtu ataweza kwenda Nairobi kutokea Dar es Salaam kwa kutumia mashirika manne ya ndani ya Afrika Mashariki ambayo ni Air Tanzania (moja kwa moja), Kenya Airways (KQ Moja kwa moja), Rwanda Air na Uganda Airlines.

Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Novemba 26, 2021 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Ladislaus Matindi alisema ndege ya kwanza itakuwa ikitoka Dar es Salaam saa 11:30 asubuhi na kuwasili Nairobi saa 12:45 kisha kugeuza saa 1:45 asubuhi na kufika Dar saa 9: asubuhi.

Ndege ya jioni itakuwa inatoka Dar es Salaam saa 2:00 jioni na kufika Nairobi saa 9:15 kisha kugeuka saa 4:15 usiku na kufika Dar es Salaam saa 5:30. Gharama ya tiketi ni Sh768, 945 kwa safari ya kwenda na kurudi na Sh483, 468 kwa safari moja.

“Tunafurahi kurejesha safari ya Nairobi ambayo ni miongoni mwa kituo muhimu hapa Afrika Mashariki na kitovu cha usafiri wa Anga,” alisema Matindi baada ya kuwasilini jijini Nairobi katika safari hiyo ya kwanza.

Advertisement

Matindi alisema safari hiyo inalenga kuwapa wateja urahisi husuani wafanyabisahara wanaofanya shughuli zao kati ya mataifa hayo makubwa kiuchumi katika ukanda huu kuweza kufanya shughuli nchi moja na kurejea nyingine jioni jambo ambalo litaepusha gharama za ziada za kulazimika kulala.

Mbali na kuimarisha urafiki wa kindugu safari hiyo inatajwa kuwa itaongeza urari wa kibiashara baina ya nchi hizo majirani, mahusiano ya kiserikali, utalii na urahisi wa wananchi kufanya safari kwenda katika mataifa mbalimbali.

Aidha Katika jitihada za kuendelea kupanua mtandao wake Novemba 18, mwaka huu ATCL ilirejesha safari yake ya jijini Lumbumbashi nchini Congo DRC kupitia jijini Ndola nchini Zambia hivyo kulifanya kulifanya kuwa na safari za kimataifa 9 kabla ya kuanzishwa kwa hii ya Nairobi.

Advertisement