Atupwa jela miezi 18 kwa kufanya kazi nchini miaka 10 kinyume cha sheria

Mshtakiwa Dishon Wanyonyi(48) (mwenye tishet ya mistari) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kuhukumiwa kwenda jela miezi 18 kwa makosa ya kuwepo nchini kinyume cha sheria na kuwasilisha nyaraka za uongo ofisi ya Uhamiaji kwa lengo la kujipatia hati ya kusafiria ya Tanzania. Picha na Hadija Jumanne
Muktasari:
- Wanyonyi anakabiliwa na mashitaka matatu ambayo ni kuwepo nchini kinyume cha sheria, kuwasilisha nyaraka za uongo ili ajipatie hati ya kusafiria pamoja na kuwadanganya maofisa uhamiaji, tukio analodaiwa kulitenda Mei 24, 2024 jijini hapa.
Dar es Salaam. Dereva wa kampuni ya Ulinzi ya SGA, Dishon Wanyonyi (48) amehukumiwa kulipa faini ya Sh1.2 milioni au kwenda jela miezi 18, baada ya kupatikana na hatia katika mashitaka matatu likiwemo la kuwepo nchini kinyume cha sheria.
Wanyonyi ambaye ni raia wa Kenya amehukumiwa adhabu hiyo, leo Alhamisi Juni 6, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukiri mashitaka yake wakati alipofikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo.
Wanyonyi ambaye ni mkazi wa Wazo, wilaya ya Kinondoni, anakabiliwa na mashitaka matatu ambayo ni kuwepo nchini kinyume cha sheria, kuwasilisha nyaraka za uongo ili ajipatie hati ya kusafiria pamoja na kuwadanganya maofisa wa uhamiaji kuhusu utaifa wake.
Hukumu hiyo, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Gwantwa Mwankuga, baada ya mshtakiwa kukiri mashitaka yake.
Mshtakiwa huyo ambaye katika utetezi wake, alidai kuwa aliingia nchini Tanzania mwaka 2005 kwa ajili ya kutafuta maisha, ametiwa hatiani kama alivyoshtakiwa na mahakama hiyo.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mwankuga amesema shitaka la kwanza ambalo ni kuwepo nchini, mahakama hiyo inamuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita.
Hakimu Mwankuga amesema katika shitaka la pili, ambalo ni kuwasilisha nyaraka za uongo ofisi ya Uhamiaji ili apate hati ya kusafiria, mahakama imemuhukumu kulipa faini ya Sh200,000 au kwenda jela miezi sita.
"Shitaka la tatu, ambalo ni kuwadanganya maofisa uhamiaji kuhusu utaifa wake, mahakama hii ina kuhukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita" amesema Hakimu Mwankuga
Hata hivyo mshitakiwa huyo ameshindwa kulipa faini hiyo na hivyo atatumikia kifungo hicho gerezani.
Hoja za awali
Mshtakiwa baada ya kukiri mashitaka yake, Wakili kutoka uhamiaji Raphael Mpuya, alimsomea hoja za awali.
Mpuya alidai, Wanyonyi aliingia nchini miaka mingi na mwaka 2014 aliajiriwa na Kampuni ya ulinzi ya SGA kama dereva huku akijitambulisha kuwa yeye ni raia wa Tanzania kwa kuwasilisha nyaraka za uongo.
Baada ya kuajiriwa, Februari 22, 2019 alitafuta cheti cha kuzaliwa cha Tanzania na kutoa taarifa za uongo kuonyesha kuwa baba na mama yake ni Watanzania, huku akijua kuwa alidanganya.
"Aliendelea kutumia cheti hicho katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na kisha kujipatia kitambulisho cha Taifa" alidai wakili Mpuya.
Hata hivyo, Mei 20, 2024 alitumia cheti hicho kujaza fomu kwa ajili ya kuomba hati ya kusafiria ya Tanzania.
“Wakati akiendelea na mchakato wa kujaza fomu hiyo, maofisa uhamiaji walimtilia mashaka na kumkamata na kumfanyia mahojiano, ambapo alikiri kuwa ni raia wa Kenya na alijipatia nyaraka hizo kwa njia ya udanganyifu" alidai Mpuya.
Alidai baada ya mahojiano, mshtakiwa alifikishwa mahakamani ha kusomewa mashtaka yake
Uamuzi wa Hakimu
Kabla ya kutolewa kwa hukumu, hakimu alimuuliza mshtakiwa iwapo ana kitu cha kusema ili mahakama imfikirie.
Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu nilikuja Tanzania muda mrefu tangu mwaka 2005 na aliyenileta alinitelekeza.
Mshtakiwa: Naomba mahakama yako inihurumie na inipunguzie adhabu.
Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, ni kweli katika hali ya kutafuta maisha na kujitafutia kazi, nilikuja nchini kinyume cha sheria, hivyo naomba mahakama yako inisamehe kwa sababu nina familia, mke na watoto wanaonitegemea.
Kwa upande wake, Wakili Mpuya aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Pia, upande wa mashitaka umedai kuwa hawana kumbukumbu za nyuma za makosa ya jinai dhidi ya mshtakiwa huyo, hivyo wanaomba apewe adhabu kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Mwankuga amesema kwa kuwa mshtakiwa amekiri mashitaka ambayo yanatengeneza makosa, hivyo mahakama imemtia hatiani kama ulivyoshtakiwa.
Akitoa hukumu, Hakimu Mwankuga amesema makosa aliyoshtakiwa nayo yana adhabu ya kifungo, faini au vyote kwa pamoja.
" Mahakama imezingatia maombi yako ya kupunguziwa adhabu, na maelezo ya upande wa mashitaka kuwa wewe ni mkosaji wa mara ya kwanza, hivyo imeona ikupe adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita kwa kosa la kwanza, kosa la pili utalipa faini ya Sh200,000 au kwenda jela miezi sita na shitaka la tatu utalipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita" amesema hakimu Mwankuga.
Mashtaka dhidi ya mshtakiwa
Mei 24, 2024 katika ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa raia wa Kenya alikutwa akiishi nchini bila kuwa na hati ya kusafiria ua nyaraka yoyote inayoonyesha uhalali wa kuishi wake.
Shtaka la pili, siku na eneo hilo, mshtakiwa akiwa raia wa Kenya aliwasilisha cheti cha kuzaliwa chenye taarifa za uongo na kitambulisho cha Taifa kwa lengo la kujipatia hati ya kusafiria ya Tanzania.
Katika shitaka la tatu, ni kuwadanganya maofisa uhamiaji kuhusu utaifa wake, ambapo siku na eneo hilo, mshtakiwa aliwasilisha fomu ya maombi kwa ajili ya kupata hati ya kusafiria ya Tanzania ikiwa na taarifa za uongo, wakati akijua kuwa yeye ni raia wa Kenya.