Auawa kwa kujaribu kuiba piki piki

Muktasari:
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ludovic Augustino Mollel (28-30) mkazi wa Lemara, jijini Arusha ameuawa na wananchi wenye hasira kali, kwa kile kilichodaiwa ni jaribio la kuiba pikipiki eneo la Sinoni.
Arusha. Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ludovic Augustino Mollel (28-30) mkazi wa Lemara, jijini Arusha ameuawa na wananchi wenye hasira kali, kwa kile kilichodaiwa ni jaribio la kuiba pikipiki eneo la Sinoni.
Mollel anadaiwa kuwa kiongozi wa kundi la watu watano, wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu katika Kata za Unga Ltd, Sinoni, Sokoni One, na Lemara.
Mtuhumiwa huyo, ameuawa kwa kipigo na kuchomwa moto usiku wa kuamkia Agosti 28 katika eneo la Barabara Kuu ya Sinoni katika Kata ya Sokoni One, jijini Arusha.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa Mount meru.
"Mwili umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital ya Mount Meru kusubiri taratibu za maziko na upelelezi wetu umeanza kupata wahusika waliotekeleza jambo hili," amesema.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa kata hiyo, Michael Kivuyo, amesema kuwa alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa mmoja wa wananchi wake, ikimfahamisha juu ya mtuhumiwa huyo kuuawa.
“Nilipigiwa simu tisa usiku kwamba kuna kijana ameuawa baada ya kuiba pikipiki ambapo walimfukuza na kumkamatia barabara ya Sinoni ambapo walimpiga na kummwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto,” amesema Diwani Kivuyo na kuongeza;
“Baada ya kusikia hivyo nilishtuka sana, na kumpigia haraka OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) ya Arusha, kumjulisha, na uzuri walikuja na maaskari kadhaa na kuuchukua mwili kuupeleka Mochwari ya Hospitali ya Mkoa Mount Meru,” amesema.