Auawa kwa kukatwa mapanga na wanawake wenzie kisa wivu wa mapenzi

Donata Amedius enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu wawili ambao ni mwanamke na mwanaume kwa tuhuma za mauaji Donata Amedeus kwa kumkatakata na mapanga kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Moshi. Donata Amedius (47), mkazi wa Kitongoji cha Kotule, Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro ameshambuliwa na kuuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wanaokadiriwa kuwa ni watano kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Mwanamke huyo alishambiliwa na wanawake wenzake ambao wanadaiwa kuwa ni watatu kwa kushirikiana na vijana wawili usiku wa Aprili 2, mwaka huu kwa kile kinachodaiwa kuwa alikuwa akitembea na mume wa ambaye miongoni mwa wanaodaiwa kutenda tukio hilo alikuwa akimtuhumu marehemu.

Inadaiwa kuwa baada ya mwanamke huyo kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake mita chache karibu na nyumbani kwake wanawake hao kwa kushirikiana na vijana hao ambao walikuwa wamejificha eneo karibu na nyumbani kwa marehemu, walichukua vijiti na kisha kumwingizia katika sehemu zake za siri na kumsababishia majeraha makubwa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kwa hatua za awali wanashikiliwa watu wawili ambao ni mwanamke mmoja na mwanaume kwa kuhusika na mauaji hayo.

"Ni kweli tukio limetokea na katika uchunguzi wetu wa awali tunawashikilia watu wawili ambao tuliwakamata siku ya tukio na taratibu nyingine za uchunguzi zinaendelea,"alisema Kamanda Maigwa.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kotule, Stephen Mboya amesema tukio hilo lilifanywa usiku wa saa nne wakati mwanamke huyo akirudi nyumbani kwake baada ya kutoka kwenye mzozo mkali wakati wakiwa wamekaa kilabuni na wanawake hao ambao walikuwa wakimtuhumu kutembea na mwanaume wa mmoja wao.

"Siku ya tukio, hawa wanawake walikuwa wamekaa mahali wanakunywa, sasa baadaye mmoja wa wanawake wale akamtuhumu marehemu kuwa alikuwa akitembea na mwanaume wake, sasa kukaibuka maneno na kutupiana chupa za bia,"

"Mwenye duka aliwataka kuondoka eneo lile kwa kuwa ilikuwa ni usiku, ambapo huyu marehemu baada ya mwenye duka kufunga alimsindikiza mpaka nyumbani kwake, sasa wakati anarejea nyumbani kwake mita chache kufika nyumbani kwake hawa wanawake pamoja na wale vijana wawili wakawa wamejificha mahali, walianza kumshambulia kwa mapanga na kumkatakata na baadaye walichukua vijiti na kumwingizia sehemu za siri," alisema Mboya.

Mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini, KCMC.