Aunguzwa na mama kwa madai ya kuiba ugali

Muktasari:

  • Mtoto Akashe Wahabi (8) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Naliendele ameunguzwa mkono na mama yake mzazi Muwaza Abeid( 29) kwa madai ya kuiba ugali na nyama.

Mtwara. Mtoto Akashe Wahabi (8) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Naliendele ameunguzwa mkono na mama yake mzazi Muwaza Abeid( 29) kwa madai ya kuiba ugali na nyama.

Ofisa ufuatiliaji na tathmini wa kituo cha msaada wa sheria Mtwara Manispaa, Judith Chitanda amelieleza Mwananchi Digital leo Julai 19, 2021 kuwa mtoto huyo aliunguzwa Julai 3, mwaka huu kisha mama yake akamficha ndani huku akimpa matibabu ya kienyeji.

"Nilipata taarifa za mtoto huyu kuunguzwa Julai 18, mwaka huu kidonda kikiwa na siku 16 na hakiko katika hali nzuri," amesema Judith.

Ameeleza kuwa baada ya kumuhoji mama Akashe ameeleza kuwa siku ya tukio mtoto alikula ugali na nyama ambao alikua amewekewa bibi yake aliyekuwa ameenda shamba.

Amesema bibi aliporudi hakukuta chakula walipouliza ndipo Akashe alikiri kuwa yeye ndie aliyekula chakula cha bibi yake.

Baada ya kukiri mama alimfunga mtoto mikono yake yote miwili kwa kutumia majani ya mnazi.

Baada ya kumfunga akachukua moto na kuanza kumtishia ndipo mtoto alipoanguka na majani ya mnazi yaliposhika moto na kumuunguza mkono wa kulia.

Mama Akashe ambaye muda wote alikuwa akilia ameomba jamii imsamehe kwa vile hakutegemea kwamba mtoto wake anaweza kuungua kiasi hicho.

"Najuta mimi sikutegemea kabisa kwamba mtoto wangu anaweza kuungua hivi, sikudhamiria kumuumiza hivi mtoto wangu ni mtundu mno na amekuwa akidokoa dokoa hata hela,"

Amesema siku ya tukio mtoto huyo alitoka kwa shangazi yake akiwa ameshakula chakula cha mchana lakini kwa vile mtoto wake ana tabia za udokozi aliamua kudokoa chakula.

Akashe amekiri kuwa mama yake huwa anampa chakula lakini siku ya tukio aliamua kuchukua chakula cha bibi yake na kula.

Afisa ustawi wa jamii wa Manispaa ya Mtwara, Godlove Miho amekiri kumpokea mtoto huyo na kumpeleka kituo cha afya cha Likombe kwa ajili ya matibabu.

"Tunaendelea na taratibu nyingine za uchunguzi kuona kama inafaa mtoto huyo kuendelea kuishi na mama yake."

Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Marc Njera amekiri kuwepo kwa tukio hilo.

Amesema tayari wamemkamata mama huyo yupo katika kituo kikuu cha polisi cha mkoa.

Afisa ustawi wa jamii amesema kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto mkoani hapo vimekithiri.