Awamu ya pili ujenzi wa JKCI kuanza Mloganzila
Muktasari:
- China na Tanzania zimetiliana saini muhtasari wa upembuzi yakinifu wa upanuzi na uboreshaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kuwa kituo bora cha magonjwa ya moyo Afrika Mashariki na kati.
Dar es Salaam. Serikali ya China na Tanzania zimetiliana saini muhtasari wa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tawi la Mloganzila ikiwemo uboreshaji wa kituo bora cha magonjwa ya moyo Afrika Mashariki na kati ambacho tayari kimejengwa.
Utiaji saini huo umefanyika leo Jumatano Januari 18, 2023 ambapo kwa upande wa Tanzania uliwakilishwa na Mganga Mkuu wa Serikali , Profesa Tumaini Nagu na ule wa China ukiwalishwa na Mshauri wa Uchumi na Biashara nchini China, Chu Kun.
Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Profesa Nagu ameishukuru Serikali ya China kwa hatua hiyo muhimu inayoleta matumaini katika kupanua na kurekebisha kituo hicho.
“Kwa niaba ya Serikali, kupitia Wizara ya Afya ninapenda kuishukuru Serikali ya watu wa China kwa tukio hili muhimu la kutia saini muhtasari wa upembuzi yakinifu, hii inaonyesha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili,” amesema Profesa Nagu.
Profesa Nagu amesema tangu Tanzania ipate uhuru, China imetoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya afya nchini Tanzania kwa kujenga mifumo na miundombinu ya afya, kusaidia huduma za msingi za afya na kuwajengea uwezo madaktari wa Kitanzania.
Aidha Profesa Nagu amesema hatua hiyo ni matunda ya ziara ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu nchini China Agosti 2018 alipotembelea nchi hiyo na kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya ya Tanzania na Tume ya Taifa ya Afya ya watu wa China.
Akieleza lengo kuu la utiaji saini wa muhtasari huo Profesa Nagu amesema, “Lengo kuu la muhtasari huu ni kuidhinisha mradi wa kuboresha na kupanua Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kufanya upembuzi yakinifu kuelekea zoezi la ujenzi. Hii itapelekea kuimarika kwa ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, hii itainua ari ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za moyo zinazotolewa kwa watu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.”
Mshauri wa Biashara na Uchumi China, Chu Kun amesema, “Huu ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili. Kwa kipindi kirefu tumekuwa tukiwachukua madaktari kwenda China kwa ajili ya kuwajengea uwezo na wa China wanakuja huku. Uboreshaji wa Taasisi ulikuwepo katika mpango tangu mwaka 2018.”
Akieleza jinsi taasisi hiyo itakavyonufaika na utiaji saini huo, Dk Peter Kisenge amesema Serikali ya watu wa China itajenga jengo kubwa katika kituo cha Mloganzila ambalo litakidhi mahitaji ya wagonjwa wa moyo nchini na hata nje ya nchi mapema mwakani.
Dk Kisenge amesema kwa sasa taasisi hiyo inapokea takribani wagonjwa 50 kila mwezi wanaotoka nchi mbalimbali kama vile Kenya, Uganda, Visiwa vya Comoro, Zimbabwe, Zaire, Malawi na Rwanda.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, James Kheri amesema hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi wa wilaya hiyo na kwamba malengo yaliyowekwa na Serikali hizo mbili lengo ni kuona mahusiano ya kidiplomasia yanaendelea hasa mambo yanayoigusa jamii.
“Mahusiano ya kidiplomasia, ujenzi wa miundombinu, utaalamu katika sehemu yetu lengo ni kuhakikisha tunajenga mji, hiki kinachokwenda kufanyika ni kuiweka Ubungo kuwa mji wa mafunzo ya kimatibabu,” amesema Kheri.