Azaki zatakiwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia

Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha LHRC, Wakili Anna Henga akizungumza  katika mkutano huo unaofanyika jijini Arusha.

Muktasari:

  • Asasi za kiraia nchini zatakiwa kusaidia watu kubadilika na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Arusha. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga ameziomba asasi za kiraia nchini, kuhakikisha zinasaidia watu wote kubadilika na kuendana na mabadiliko  ya  teknolojia (TEHAMA) ili kuleta matokeo chanya katika ulimwengu.

Henga ameyasema hayo leo Oktoba 27 jijini Arusha katika Kongamano la Wiki ya Azaki linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha na kuwakutakutanisha wadau mbalimbali wa asasi za kiraia.
Amesema kuwa, dunia inabadilika na kila mmoja wao anapaswa kubadilika ila kwa kuhakikisha asasi inabadilika na watu wote bila kubagua wasomi na wenye uwezo.

"Nawaomba Azaki tubadilike tuendane na mabadiliko ya TEHAMA ili teknolojia hii isituache nje na tunapobadilika tubadilike na watu wote bila kubagua  watu ili kuleta matokeo chanya katika jamii,"amesema.
Amesema kuwa, Azaki zinafanya kazi kubwa katika jamii za aina mbalimbali na hivyo zinapaswa kuendelea kubaki ili kusaidia watu katika upatikanaji wa haki za kiuchumi,kiraia,kusikilizwa na nyingine nyingi.
Amesema kuwa, haki ya kusikilizwa ni muhimu na ili mtu aweze kupata huduma  za kijamii ni lazima asikilizwe.
Pia amezitaka asasi hizo kuitambua fedha sio msingi wa maendeleo bali lazima wananchi wakubaliane kitu wanachokiamini watatoa ushirikiano.
"Unajua mradi ukiendelea katika jamii  wananchi wapo tayari kujitolea kwa hali na mali ikiwemo  fedha na hata ikitokea mfadhili amejiondoa mradi utaendelea sababu wananchi wameshirikishwa  na wameona kile kinachofanyika ni chao,hivyo kikubwa hapa ni ushirikishwaji wa wananchi katika kila jambo linalotakiwa kufanyika"amesema.

Amehimiza katika utawala bora, umuhimu wa kuandaa vijana kwenye utendaji kazi wao, maana wao ni wepesi katika mabadiliko ya teknolojia tofauti na mtu mzima, kadri umri unavyokùwa mkubwa mambo mengi yanamtupa nje.