Baba ambaka mwanae wa miaka 15, ampa ujauzito

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa mtoto huyo, mama yake ana mtoto mdogo ambaye huwa anampeleka kliniki kila mwezi, hivyo baba huyo mlezi alikuwa akitumia nafasi hiyo kutekeleza uhalifu huo

Mtwara. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linamshikilia Said Mapesa (42) kwa kosa la kumbaka mtoto wa mke wake mwenye umri wa 15 na kumpa ujauzito.

Akizungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake leo Aprili 5, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amesema jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa likiendelea na uchunguzi kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

“Ni kweli tukio limetokea na pia tunaye mtuhumiwa ambaye alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15 na kumpa ujauzito.

“Tukio hilo limetokea wilayani Newala n tumeshamkamata mtuhumiwa. Hilo ni kosa la jinai, upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani,” amesema Suleiman.

Mwananchi imefika nyumbani kwa bibi wa mtoto huyo na kufanya naye mahojiano ambapo amesema mtoto huyo amesema mimba hiyo amepewa na baba yake mlezi, ambaye kwa sasa amemfukuza.

Amesema amekuwa akimtishia na kumtaka asimwambie mama yake kabla ya kumbaka huku akimuahidi kumnunulia nguo na kumpa pesa.

Kwa mujibu wa mtoto huyo, mama yake ana mtoto mdogo ambaye huwa anampeleka kliniki kila mwezi, hivyo baba yake alikuwa akitumia nafasi hiyo kutekeleza uhalifu huo.

“Siku hiyo nilikuwa naosha vyombo, baba akaja akaniita nimfuate ndani, nilipofika ndani alinishika na kuanza kunifanyia tendo hilo, tena chumbani kwake na nyumbani hakukuwa na watu na alinionya nisimwambie mama, yaani ulikuwa ndiyo mchezo wake.

“Kuna siku nilijaribu kumwambia mama naye alimfuata baba kumuuliza na baba alikataa kuwa hajawahi kufanya hivyo, jambo ambalo lilinifanya nikose utetezi.

 “Wala sikujua kama baba amenipa mimba, lakini nilianza kuona tumbo linakuwa kubwa, nilimwambia mama ambapo alibaini kuwa nina ujauzito, baada ya kugundulika hivyo baba aliniletea majani akataka nitoe mimba, nilikataa lakini alinilazimisha, nikanywa kidogo nikaona ni chungu sana nikaamua kuacha kabisa kuinywa, nikaimwaga. Hata nilipomwambia mama hakuchukua hatua zozote,” amesimulia mtoto huyo.

Bibi wa mtoto huyo amesema ameshangazwa na hatua ya mama huyo kupata taarifa ya mtoto kubakwa lakini hakuchukua hatua zozote.

“Mjukuu wangu alikuwa akiishi kwa mama yake mzazi lakini alifukuzwa na baba huyo baada ya mama yake kuondoka nyumbani, akaja kwangu. Nilijaribu kuwaita lakini hawajafika, huyu mtoto ni mdogo sana kwa umri wake,” amesema bibi huyo.