Baba jela miaka 30 kwa kumnajisi mwanaye wa miaka sita

Mkazi wa Kisesa Wilaya ya Magu, Nurdin Abdalah (54) akisubiri kuingizwa kwenye chumba cha mahabusu ya Mahakama ya Wilaya ya Magu muda mfupi baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto wake mwenye umri wa miaka sita. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Kifungo cha miaka 30 jela alichohukumiwa Nurdin Abdallah anayejihusisha na biashara ya kuuza vitabu vya dini kimetokana na ushahidi wa mashahidi sita waliofika mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Magu.

Mwanza. Nurdin Abdallah (54), mkazi wa Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza amehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wake (jina lihahifadhiwa) mwenye umri wa miaka sita

Hukumu hiyo imetolewa leo Aprili 21, 2023 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya ya Magu, Erick Kimaro baada ya kuridhika na ushahidi  wa mashahidi sita wa upande wa Jamhuri uliowasilishwa mahakamani hapo katika shauri la jinai namba 79/2022.

"Kutokana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri, Mahakama hii imeridhika bila shaka yoyote kuwa mshtakiwa ulitenda kosa analoshtakiwa nalo, inamtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela. Nafasi ya kukata rufaa iko wazi kwa upande wowote ambao haujaridhika na uamuzi huu,” amesema Hakimu Kimaro

Miongoni mwa mashahidi walioitwa mahakamani ni pamoja na Daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto anayedaiwa kubakwa ambaye amethibitisha kubaini michubuko katika sehemu za siri za mtoto huyo ambaye pamoja na wenzake wanaishi na baba yao baada ya kutengana na mama yao.

Baada ya hukumu hiyo, aliyekuwa mshtakiwa huyo aliwekwa chini ya ulinzi na maofisa wa Jeshi la Polisi tayari kwa kupelekwa gerezani kuanza kutumikia adhabu yake.

Awali, akisoma maelezo ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nuru Julius aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kwa nyakati tofauti Mei, 2022 kinyume na Kifungu namba 130 (2) (e) cha Kanuni ya Adhabu.

Mwendesha Mashtaka huyo ameiambia Mahakama kuwa tukio la mtoto huyo kubakwa liligunduliwa na majirani ambao walilifikisha Kituo cha Polisi Kisesa kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa.

Akijitetea kabla ya kuhukumiwa kifungo jela, Nurdin anayefahamika zaidi mitaani kwa jina la Mwinjilisti kutokana na shughuli yake ya kuuza vitabu vya kidini aliomba kupunguziwa adhabu akisema ana watoto wanne na mdogo wake mgonjwa ambao wote wanamtegema kwa huduma na mahitaji yote.