Bado ni vuta nikuvute mkataba uwekezaji bandari

Dar es Salaam. Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa mkataba wa makubaliano ya uendeshaji na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, huku ikisema kwamba, itasaidia kuongeza ufanisi na kukuza pato la Taifa.

Hata hivyo, bado baadhi ya wadau wameendelea kuukosoa mkataba huo, akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, aliyeshauri kufanyiwa kazi kwa vipengele vinavyokanganya.

Mkataba huo wenye ibara 31 ulisainiwa Oktoba 25, mwaka jana baina ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari pamoja na maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Tayari Juni 10, mwaka huu Bunge lilipitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba huo, kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini.

Hata hivyo, kumekuwepo na mvutano kuhusu baadhi ya vipengele kwenye mkataba huo ambapo, wadau mbalimbali wamedai kuwa havina tija, huku wengine wakienda mbali kwa kudai kuwa bandari imeuzwa.

Kutokana na hofu hiyo, mara kadhaa Serikali kupitia watendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na hata Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wamekuwa wakitoa ufafanuzi kuhusu wasiwasi huo. Mapema wiki iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kuwa maoni yote yaliyotolewa na wadau mbalimbali yatakwenda kufanyiwa kazi kwa uzito na kwamba, hakuna yatakayopuuzwa.

Msemaji wa Serikali

Lakini jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kwa mara nyingine alisema kuwa Serikali haiwezi kukaa kimya kuona Watanzania wanapoteza mapato wakati uwezekano kupata mapato kupitia bandari upo.

“Tuna bandari yetu hapa ambayo tunaambiwa hivi sasa inahudumia bajeti yetu kwa asilimia 37, tukifanya uwekezaji huu inaweza kuhudumia bajeti ya Serikali kwa asilimia 67.

“Unatoka kwenye Sh7.7 trilioni unakwenda kupata Sh26.7 trilioni. Watanzania tunataka nini? Watu wanasema vipengele vya mkataba, hakuna kipengele chenye matatizo,” alisema Msigwa.

Alisema ushirikiano huo unakwenda kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania na kwamba, madai kuwa bandari inakwenda kuuzwa hayana ukweli na wananchi wayapuuze.

Alisema kwa sasa bandari imekuwa haijiendeshi kwa ufanisi kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo hujuma zinazofanywa, mojawapo ikiwa kuchezea mifumo, hivyo kuingia kwa mwekezaji kutakwenda kumaliza tatizo hilo na ufanisi wa bandari utaonekana.

Akifafanua zaidi, Msigwa alibainisha kuwepo upigaji unaotokea bandarini kwa kiasi kikubwa, kuwa unasababishwa na changamoto kwenye mifumo na ndiyo sababu ya kuharakisha uwekezaji huo wenye teknolojia ya hali ya juu, ili kudhibiti hali hiyo inayolipotezea fedha Taifa.

“Tunakwenda kuangalia namna ya kuboresha mifumo kwenye bandari yetu. Sasa hivi kumekuwa na upigaji mkubwa, tafiti zinaonyesha upigaji bandarini kwa sehemu kubwa unasababishwa na changamoto za kimfumo, kwa hiyo hii kampuni tunaingia nayo makubaliano lengo letu likiwa kuimarisha mifumo ya bandari,’’ alisema na kuongeza:

“Tunakwenda pia kuweka namna bora ya kuhudumia mizigo kwa haraka, tunataka tufikie hatua meli ikiingia bandarini, ihudumiwe ndani ya siku moja.’’

Kuhusu wafanyakazi bandarini, Msigwa alisema hakuna atakayepoteza kazi na kutakuwa na ajira nyingine mpya kutokana na wigo mpana wa huduma zitakazokuwa zinatolewa.

Jaji Warioba afunguka

Hata hivyo, akizungumza juzi na kituo cha televisheni cha Azam, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alishauri kuangaliwa upya kwa vifungu vyenye mkanganyiko katika mkataba huo.

Jaji Warioba alisema ni kweli uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam haukuwa wa kuridhisha kwa muda mrefu, lakini makubaliano yaliyopo yana vipengele vinavyoleta wasiwasi.

“Nimeusoma huo mkataba wa makubaliano. Niliamini kwa sababu sio mara ya kwanza tumekuwa na mikataba ya aina hii, tumekuwa na mikataba hii katika maeneo mbalimbali. Sasa tunapofanya hii mikataba tujifunze huko nyuma upungufu gani ulikuwepo.

“Ni kweli kwamba mkataba ule una vipengele ambavyo vingezua hofu, hili tusilikwepe, tuliangalie tuone tutakavyoweza kuboresha hiyo,” alisema.

Jaji Warioba, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema hakukuwa na maandalizi ya mapema katika kuingia mkataba huo.

“Nadhani tumechelewa katika utaratibu huu, kwa sababu tulikuwa na TICTS (Tanzania International Container Services) pale, tulijua mwisho wake umefika, tungejua tungefanya mapema, kwa sababu bandari ni muhimu sana,’’ alisema.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya aliyefanya mahojiano na Mwananchi mwishoni mwa wiki, alisema miongoni mwa maeneo yanayotia hofu ni kutokuwekwa wazi mapema kwa mkataba huo ili kama kuna anayetaka kuwekeza ajitokeze.

Alisema kwenye tangazo hilo, Serikali ilitakiwa kubainisha sifa za mwekezaji anayetakiwa kwenye uwekezaji huo.

“Utaratibu wa zabuni haukufanyika, limeenda kimya kimya, kama wangetangaza, Uingereza wangetaka kuja kuwekeza, Marekani nao wangetaka, wote wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi hiyo,” alisema Ngawaiya.

Hata hivyo, wakati akisoma azimio la kuridhiwa kwa makubaliano hayo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali ilipokea maombi ya kampuni mbalimbali kubwa kuomba ushirikiano huo, lakini walichagua kuanzisha majadiliano na DP World kutokana na uwezo na uzoefu wake katika uendeshaji wa bandari duniani.

Mbali na Ngawaiya, wadau wengine waliunga mkono mkataba huo huku wakieleza kwamba hatua hiyo itakuwa na manufaa kwa Taifa, hasa kwa kuzingatia manufaa ambayo yatapatikana baada ya mwekezaji huyo kuanza kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya mabadiliko ya wanawake na vijana Tanzania (Tafeyoko), Elvice Makumbo alisema mkataba huo una manufaa na kwamba suala hilo siyo la wanasiasa au viongozi wa dini, bali ni la Watanzania wote.

“Tunawaomba Watanzania tusilifanye jambo hili la mkataba wa bandari kuwa kichaka cha kupenyeza mambo yetu ya siasa na uongozi, hasa kwa wanasiasa na vyama vya siasa. Kwa kufanya hivyo tunapotosha azma nzima ya jambo hili na kuleta taharuki kwenye nchi,” alisema.


Imeandikwa na Peter Elias, Elizabeth Edward na Emmanuel Msabaha