Bakwata yafanya uzinduzi wa awali msikiti mkubwa Dar

Muktasari:

  • Baraza kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), leo Aprili 15, 2022 limefungua msikiti wake uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kuanza kutumiwa na waumini wa dini ya kiislamu kwa ajili ya ibada.


Dar es Salaam. Baraza kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), leo Aprili 15, 2022 limefungua msikiti wake uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam kuanza kutumiwa na waumini wa dini ya kiislamu kwa ajili ya ibada.

Msikiti huo uliojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Morocco, ndiyo mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia chumba cha ibada cha msikiti huo kinachochukua waumini 8,000 kwa wakati mmoja, maktaba, ukumbi wa mikutano, vifaa vya utawala, maegesho ya magari, duka kubwa na maeneo ya bustani.

Katika hafla ya ufunguzi wa msikiti huo iliyofanyika leo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Aboubakar Bin Zubeir, amesema kilichofanyika kinatoa ruhusa kwa waumini wa dini hiyo kuutumia kufanya ibada wakati uzinduzi rasmi unasubiriwa.

"Ufunguzi huu wa awali ni ombi la Rais Samia Suluhu Hasaan kwa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI la kutaka waislamu tuutumie kufanya ibada kabla ya uzinduzi rasmi," amesema.

Amesema uzinduzi rasmi utahudhuriwa na Mfalme wa Morocco, akiahidi sherehe zaidi zitafanyika siku hiyo ambayo bado haijapangwa kuwa lini zitafanyika.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Bakwata, Sheikh Mataka amesema hiyo ni fursa kwa waumini wa dini hiyo kufanya ibada katika msikiti huo.

"Hasa kwa mwezi huu wa Ramadhani kwa mujibu wa matakwa ya dini yetu tunapaswa kuwa karibu na Mungu, hivyo kufunguliwa kwa msikiti huu kutafanya waumini waswali kwenye mazingira mazuri," amesema.

Kujengwa kwa msikiti huo ni baada ya ombi la aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli la kutaka nyumba hiyo ya ibada kwa waumini wa kiislamu ijengwe nchini.

Mbali na msikiti huo, pia Tanzania na Morocco zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika elimu ya jadi, misingi ya dini, ujenzi na usimamizi wa misikiti, kubadilishana uzoefu, na aina nyingine za ushirikiano unaolenga kuhifadhi maadili halisi ya Kiislamu na kusaidia kuzuia upotoshaji katika dini hiyo.