Balozi Possi ataka fursa zaidi kukuza utalii
Muktasari:
- Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi ameshauri kuongeza utalii wa mijini, akitaka wadau hasa Bodi ya Utalii, Mamlaka za miji kuweka sawa historia za miji maeneo yaelezwe vizuri ili watu wanaotaka watembelee.
Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi amesema Tanzania inazo fursa nyingi za kukuza utalii zaidi ya mbuga za wanyama na fukwe na milima.
Balozi Possi ameyasema hay oleo Septemba 27 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space, akisema ipo haja ya kutanua wigo wetu mfano katika maeneo ya utamaduni.
“Kwa nini kijiji cha Makumbusho pekee ndiyo mtu aweze kupata utalii wa utamaduni, wakati Tanzania ina utajiri na wakati kila mkoa ungefaa kuwa na makumbusho wa kiutamaduni?” amehoji.
Ameshauri pia kuongeza utalii wa mijini, akitaka wadau hasa Bodi ya Utalii, Mamlaka za miji, kuweka sawa historia za miji maeneo yaelezwe vizuri ili watu wanaotaka kwenda kutembea watembee.
“Kuna haja pia ya kutafakari namna tunavyotangaza utalii wetu kwa kuangalia nani anafanya nini, tuangalie Bodi ya Utalii ifanye nini, Wizara ya Maliasili na utalii ifanye nini kwa sababu nimeona kumekuwa na muingiliano wa majukumu na kufanya coordination kuwa si nzuri,” amesema.
Kuhusu sekta binafsi, ameshauri zisaidie kupunguza gharama za utalii, ili mtalii mmoja akimlipa wakala mmoja wa utalii Tanzania awe na uwezo wa kwenda mikoa tofauti kama , Ruvuma, Arusha pamoja na Visiwani Zanzibar.
“Kuna gharama nyingine haziwezi kupunguzwa mfano mtu anatoka Marekani kwa ndege hadi Serengeti ni tofauti na mtu anayetoka Uganda hadi Kilimanjaro, umbali ule pekee ni gharama haiwezi kupunguzwa
“Lakini kuna gharama za ndani, huenda hapa ni suala la sekta binafsi na za umma kukaa kuangalia maeneo ambayo yakifanyiwa kazi gharama za malazi zinaweza kupungua kwa sababu mtu ambaye anakwenda kuangalia wanayama Serengeti hamu yake siyo kulala hotelini bali kuona wanyama,” amesema.
Akizungumza katika mjadala huo, mkuu wa Chuo cha utalii Tanzania (NCT) Dk Florian Mtey tayari wameshachukua hatua kutoa mafunzo ya muda mfupi ambapo wameanza kutoa mafunzo kwa maofisa uhamiaji 412 kutoka Tanzania bara na Visiwani.
“Wiki iliyopita tumesaini mkataba na Jeshi la polisi Tanzania ili katika mitaala ya vyuo vyao vya jeshi tutaingiza moduli za utalii na ukarimu,” amesema Dk Mtei.
Amesema wanafanya hivyo ili waweze kufahamu kwa undani aina ya huduma wanazostahili wateja na wakikutana na wateja wawahudumie vipi.
“Tumeanza na uhamiaji kwa sababu sehemu wanazoingilia watalii huwa wanakutana na uhamiaji pia usalama wao wakiwa nchini wasisumbuliwe,’ amesema.
Ameyasema hayo wakati akichangia mada isemayo Nini kifanyike kuongeza idadi ya watalii nchini tukiadhimisha siku ya utalii duniani.