Bangi zawapeleka wawili jela miaka 20
Muktasari:
Washtakiwa hao wawili wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja kwenye kesi mbili tofauti zilizosomwa hukumu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Babati. Watu wawili wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Babati mkoani Manyara kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya na kuzisafirisha kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa Februari 15, 2023 na Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Victor Kimario baada ya washtakiwa kukiri makosa yao.
Waliohukumiwa kifungo ni Swalehe Mohamed (27) mkazi wa Mdori wilayani Babati na Yahaya Bakari (37) mkazi wa Ngaramtoni jijini Arusha.
Kimario amesema katika kesi namba 21 ya mwaka 2023 Swalehe Mohamed alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kupatikana na misokoto 125 ya bangi sawa na gramu 450.
Amesema mshtakiwa alikutwa na misokoto hiyo Desemba 29 mwaka 2022 akiwa nyumbani kwake Mdori misokoto ikiwa chumbani.
Hakimu amesema mshtakiwa alikiuka Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa ya Kulevya kifungu cha 15 A (1) (2) (C) ya mwaka 2005 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Mshtakiwa huyo amefikishwa mahakamani Februari 15 na kusomewa shitaka lake na kukiri maelezo yanayotengeneza shitaka hilo ndipo akatiwa hatiani.
Katika kesi namba 19 ya mwaka 2023 iliyokuwa inawakabili washtakiwa wawili Yahaya Bakari (37) mkazi wa Ngaramtoni jijini Arusha na Frank Mushi (45) mkazi wa Sakina jijini Arusha kwa kosa la kusafirisha mirungi bunda 247 sawa na kilogramu 94.85 mshtakiwa namba moja Bakari ametiwa hatiani na kufungwa kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kukiri makosa na mwenzake ataendelea na kesi hiyo Februari 16 mwaka huu.
Akitoa hukumu hiyo hakimu amesema washtakiwa hao walikamatwa Februari 2 mwaka 2023 katika Kijiji cha Bonga wilayani Babati walikuwa wakisafirisha mirungi kwa kutumia gari lenye Fuso ambalo ni kampuni ya Kisare.
Kimario amesema washtakiwa hao walikiuka sheria ya kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya kifungu cha 15 A (1) (2) (C) ya mwaka 2005 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Kabla ya hukumu hiyo wakili wa serikali kutoka ofisi ya Taifa ya mashtaka John Aloyce amesema washtakiwa hawana rekodi ya makosa ya uhalifu hivyo mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.
Kwa upande wake, Yahaya Bakari ameiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea na mtoto wake anaumwa degedege na anaishi na bibi yake, huku Swalehe Mohamed akiomba huruma ya mahakama kwa kuwa ana familia inamtegemea pia.