Bashe apeleka kicheko kwa wakulima wa shayiri

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo Hussen Bashe ametangaza neema kwa wakulima wa shayiri akiwataka kuongeza uzalishaji zaidi kwani wamepata soko la uhakika.

Dodoma. Waziri wa Kilimo Hussen Bashe ametangaza neema kwa wakulima wa shayiri akiwataka kuongeza uzalishaji zaidi kwani wamepata soko la uhakika.

Bashe ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 7, 2023 kufuatia makubaliano ya kimkataba kati ya kiwanda cha Kilimanjaro ambapo wanalenga kupunguza uagizaji wa zao la shayiri kutoka nje kama ilivyokuwa.

Mpango huo unakwenda kusaidia uzalishaji wa zao hilo katika mikoa ya Mbeya, Rukwa, Manyara na Kilimanjaro kufikia tani 32,000 baada ya miaka mitatu.

Bashe amesema, kuanzia mwezi Machi mwakani, Tanzania haitaagiza shayiri kutoka nje kwa ajili ya viwanda vyake badala yake itategemea shayiri kutoka kwa wakulima wa ndani watakaolisha viwanda.

Amesema ilikuwa ni aibu kuagiza shayiri kutoka nje kwa ajili ya kulisha viwanda vya ndani wakati ardhi ya kilimo ipo ya kutosha na kwmba sasa wameamka.

Waziri Bashe amesema wameingia makubaliano ambayo hayatakuwa na mabadiliko ya kisera ambayo itakuwa na utozwaji wa kodi kwa viwango tofauti kwa shayiri inayoagizwa kutoka nje na inayozalishwa ndani ili kuwalinda wawekezaji na viwanda vyao.

Amesema kwa muda mrefu wakulima wa shayiri walikosa soko la zao hilo wakati na iliwakatisha tamaa hata kwenye uzalishaji jambo lililowasumbua Serikalini ingawa sasa wanaamini kuwa wamefanikiwa.

Ametaja mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Rukwa na Mbeya na ndiyo itakayoingiza kiwandani shayiri ya kutosha na wanategemea kuwa viwanda vitapata malighafi ya kutosha.

“Tanzania inaingiza kwa kiasi kikubwa shayiri kutoka nje, kwa hiyo tuliomba kutoka kwa wenzetu Wizara ya Fedha waangalie kwenye suala la kodi la wakakubali sasa leo tunakwenda kuhitimisha safari hii ili kutengeneza ushindani wa kweli,” amesema Bashe.

Katika hatua nyingine Waziri amesema baada ya kupata soko la shayiri, sasa wanaelekeza nguvu zao kwa wakulima wa zabibu Dodoma ili wapate soko la uhakika kwa kuuza mchuzi wao moja kwa moja badala ya kupitia Cetawico.

Mkurugenzi wa Tanzania Breweries Limited (TBL) Jose Moran amesema wamejidhatiti kununua mazao ya wakulima kwa bei itakayowapa ari ya kuzalisha zaidi na kuongeza thamani.

Moran ameomba ushirikiano na wakulima katika uzalishaji wa shayiri akitaka uwe mkubwa kwani wanategemea kuongeza nguvu ya uzalishaji wa vinywaji vitokanavyo na shayiri na hivyo kukuza soko.