Waziri Bashe asitisha mgogoro wa Tari na Wananchi Mbeya

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza na wakazi wa Sae jijini Mbeya baada ya kufika kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 49 baina ya Wananchi na Taasisi ya Utafiti Tari. Picha na Hawa Mathias

Mbeya. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesitisha zoezi la ujenzi wa mpaka na nyumba za makazi eneo la Sae jijini Mbeya baada ya kuibuka kwa  mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 49.

Mgogoro huo unahusisha  eneo lenye ukubwa hekari 67 baina ya Wananchi na  Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari -Uyole) jijini Mbeya.

Bashe amesitisha mgogoro huo jana June 3, 2023 kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi  uliofanyika katika Mtaa wa Sae Kata  ya Ilomba ambapo aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera .

“Nimesitisha zoezi la ujenzi wa makazi na uzio uliokuwa ukiendelea katika eneo linalomilikiwa na Tari kwa sasa nahitaji kupata idadi ya watu 800 waliokuwa ndani ya eneo hili kabla ya Wizara haijachukua hatua za kulipa fidia au kurejesha eneo hilo,”amesema.

Aidha Waziri Bashe amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa kuwasilisha taarifa za takwimu za watu walioathirika katika eneo hilo sambamba na eneo hilo kutoendelezwa kwa makazi.

“Hili eneo linaendelezwa kwa makazi tunaangalia tu, sasa hata kama Wizara itataka kurejesha hizo hekari 67 lazima utaratibu ufuatwe na kwa sasa nasitisha shughuli za ujenzi wa uzio na makazi,”amesema.

Bashe amesema amepokea ombi kwa Spika na Mbunge wa Mbeya Mjini na atawasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mwenye mamlaka.

“Ombi lenu Mbunge ameniambia sio leo wala jana ila nikipata ridhaa ntarejea tena, kama ni kulipa fidia kulingana na thamani ya ardhi kwa miaka ya sasa na halitachukua muda kabla ya maonyesho ya nane nane mtapata majibu,”amesema Bashe.

Awali akizungumza kwa niaba ya Wananchi, Dk Tulia amesema mgogoro huo umedumu kwa miaka mingi na kwamba ufike wakati Serikali kufanya maamuzi sahihi ili wananchi wajue hatma yao.

“Ufike wakati Serikali ilimalize jambo hili ambalo limedumu kwa muda mrefu ili kila upande ikiwemo Wananchi  wapate stahiki zao sambamba na kuachiwa maeneo yao ama kulipwa fidia lakini ombi la wananchi ni kuachwa na sio kuondolewa,”amesema  Dk Tulia.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amesema eneo hilo lina hati ya Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) .

Mwenyekiti mtaa wa Sae, Elius Mwakyusa amesema mgogoro huo umekuwa ukiwapa vitisho vya kuwataka kuondoka katika eneo hali iliyowafanya kupaza sauti kwa Mbunge wao.

“Zaidi ya miaka 40 hili eneo wananchi tunaendeleza makazi, tunashindwa kuelewa leo hii Serikali inaibuka na kutaka tuondoke, jamani nchi hii ni ya kwetu sote na Rais Samia Suluhu Hassan anataka haki itendeke,”amesema.