Basil Mramba akumbukwa kwa mambo mengi
Muktasari:
Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Basil Mramba atakumbukwa kwa mambo manne aliyoyafanya wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu akiwa mshauri wa Rais katika masuala ya fedha na uchumi.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Basil Mramba atakumbukwa kwa mambo manne aliyoyafanya wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu akiwa mshauri wa Rais katika masuala ya fedha na uchumi.
Godfrey Mramba, ambaye ni mtoto wa marehemu, alisema Mramba alifariki dunia jana katika Hospitali ya Regency alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na maradhi ya Uviko-19.
Katika utumishi wake, Mramba alifanya kazi kubwa wakati wa utawala wa Hayati Benjamin Mkapa, kipindi ambacho Serikali ilikuwa ikitekeleza sera mpya ya ubinafsishaji na ndiyo kipindi utandawazi ulikuwa unashamiri.
Miongoni mwa mambo aliyoyasimamia akiwa Waziri wa Fedha na Uchumi kati ya mwaka 2001 – 2005, ni kuinua uchumi wa Tanzania uliokuwa umeporomoka.
Soma zaidi: Basil Mramba afariki dunia kwa Uviko-19
Pia, alifanya kazi ya kuvutia uwekezaji nchini na kuhakikisha nchi inanufaika.
Mramba alishiriki kuzishawishi taasisi za fedha za kimataifa kuisamehe Tanzania madeni yake yaliyokuwa mzigo kwa Serikali na kufanikiwa kupunguza deni la Taifa kwa karibu asilimia 50.
Pia, Mramba atakumbukwa kwa msimamo wake katika ununuzi wa ndege ya Rais ulioibua mjadala mzito nchini.
Alisimama imara mpaka ndege hiyo ikanunuliwa kwa ajili ya safari za mkuu wa nchi.
Katika kutetea hoja ya ununuzi wa ndege ya Rais, Mramba alitoa kauli akisema: “Watanzania tuko tayari kula nyasi ilimradi ndege ya Rais inunuliwe,” kauli iliyoonekana kuwakera baadhi ya watu, ilisisitiza umuhimu wa nchi kuwa na ndege ya Rais.
Jambo jingine litakalomfanya Mramba akumbukwe ni kuanzisha Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) akiwa mkurugenzi wake wa kwanza. Shirika hilo lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 28 ya Mwaka 1973 na Mramba aliliongoza kwa ufanisi mkubwa.
Wastaafu wamlilia
Waziri Mkuu mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye alisema Mramba alikuwa kiungo katika harakati za kufufua uchumi wa Taifa baada ya kukabidhiwa jukumu la kuongoza Wizara ya Fedha.
Alisema katika kipindi hicho, Serikali ilikuwa na hali mbaya kiuchumi na wakaamua kuendesha mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kwa lengo la kushawishi kufutiwa mzigo wa madeni chini ya marehemu Mramba.
“Nimesikitika sana kwa kweli, nimeumia sana. Kwenye utumishi wake alisaidia sana, akiwa na wazo la kushauri anawasilisha haraka ngazi ya vikao, ndio alisaidia kusamehewa madeni na mashirika ya IMF na Benki ya Dunia kwa kukutana nao, walimkubali sana,” alisema Sumaye huku akimkumbuka kwa uwazi.
Jambo jingine analokumbuka Sumaye kwa Mramba alisema alikuwa mcheshi na kiongozi aliyependa utani mara kadhaa, huku kada mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Anna Abdallah akidai kumpoteza kiongozi wa rika lake katika ngazi ya wizara chini ya Serikali ya Awamu ya Pili na Tatu.
“Nakumbuka Serikali ya Awamu ya Pili alikuwa Waziri wa Viwanda, halafu mimi nikiwa Waziri wa Tamisemi; baadaye Awamu ya Tatu nikapelekwa Wizara ya Ujenzi yeye (Mramba) akiwa Waziri wa Fedha, alikuwa na mchango mkubwa sana hata kwenye vikao alionekana kujua mambo mengi,” alisema Anna, aliyeguswa na mchango wake katika uanzishaji wa Sido.
“Lakini jambo kubwa nakumbuka alipenda sana kushirikiana na wenzake, kama kuna jambo atakufuata wizarani mtazungumza, nimesikitishwa sana na kifo chake.”
Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi katika Awamu ya Nne, alisema anamkumbuka marehemu Mramba kama kiongozi mchapakazi aliyethamini zaidi utendaji wa kazi zake.
“Nilimfahamu kwa wakati huo, mimi nilikuwa msaidizi wa Rais Mwinyi (Rais Ali Hassan Mwinyi) kabla ya Mkapa (Rais Benjamini Mkapa) Awamu ya Tatu, sikuwa naye karibu lakini ninamkumbuka alikuwa mcheshi kiasi na kwenye kazi hapendi utani,” alisema Balozi Sefue.
Kiongozi mwingine aliyeguswa na msiba huo ni Cleopa Msuya, Waziri Mkuu mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Pili na Tatu aliyemtambua kama kiongozi aliyetumikia nafasi yake kwa uchapakazi baada ya kutoka masomoni.
“Alikuwa kiongozi mzuri sana, ni Watanzania waliosomeshwa na baadaye nakumbuka alikuja kuanzia Sido, baadaye akaingia bungeni kisha kuanza kutumikia nafasi za waziri hadi alipostaafu,” alisema.
Msiba nyumbani kwake
Hali ya ukimya ilionekana kutawala nyumbani kwa marehemu Mramba. Mwananchi ilifika nyumbani kwake na kushuhudia watu wachache walioingia ndani ya uzio wa nyumba hiyo huku geti likifungwa na kila aliyeingia alihojiwa.
Awali, taarifa iliyotolewa na mtoto wa marehemu, Godfrey ilieleza kuwa familia inahitaji faragha kwenye msiba huo, hivyo wangeruhusu ndugu pekee.
Alisema hilo limefanyika kutokana na hali ya sasa ya ugonjwa wa Uviko-19, hivyo, wasingependa kuwepo na mkusanyiko.
Nje ya makazi ya Mramba yaliyopo Masaki Barabara ya Mawenzi, yalionekana magari machache. Baadhi ya watu walioingia kwenye nyumba hiyo walionekana kutoka ndani muda mfupi.
Mlinzi aliyekuwa mlangoni alikuwa akimhoji kila aliyeingia na hata waandishi walipojaribu kuingia aliwazuia.
Kesi yake na hukumu
Mramba na wenzake walikabiliwa na tuhuma kati ya Agosti 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart Government Business Assayers ya Uingereza kinyume cha sheria.
Julai 7, 2015, Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona walihukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh5 milioni baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.5 bilioni.
Hata hivyo, Februari 6, 2016, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwabadilishia adhabu viongozi hao wastaafu na kuwa kifungo cha nje wakiwa tayari wametumikia miezi saba gerezani.
Imeandikwa na Peter Elias, Kelvin Matandiko, Elizabeth Edward, James Magai na William Shao