Bavicha yawasilisha ombi kwa Ndugai kuhusu kina Mdee
Muktasari:
- Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza umma agizo lake la kumtaka katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika kuwasilisha tena taarifa za kufukuzwa uanachama wabunge 19 amelitoa kwa mujibu wa kanuni ipi.
Moshi. Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza umma agizo lake la kumtaka katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika kuwasilisha tena taarifa za kufukuzwa uanachama wabunge 19 amelitoa kwa mujibu wa kanuni ipi.
Wabunge 19 akiwemo Halima Mdee walifukuzwa uanachama Chadema Novemba 2020 lakini Ndugai amesema hana maelezo ya kina kuhusu kufukuzwa kwao na akakitaka chama hicho kimjulishe kwa taarifa rasmi za vikao vilivyotoa uamuzi huo.
Mdee na wenzake walifukuzwa uanachama baada ya kwenda kuapishwa bungeni kuwa wabunge wa viti maalumu wakati chama hicho hakikuwateua.
Bavicha leo Jumapili Mei 9, 2021 imesema wanafahamu kuwa kamati ya kudumu ya kanuni za Bunge haikuwahi kukaa na kulizungumzia jambo hilo wala kupigiwa kura na wabunge.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Kaimu Mwenyekiti wa Bavicha, Moza Ally amesema kinachofanywa na Ndugai ni ukiukwaji na kinyume cha Katiba kwa kuwa Mdee na wenzake wamepoteza sifa za kuwa wabunge.
"Spika amesema barua ya katibu mkuu haitoshi kumpa taarifa za uamuzi ya chama, yeye alitaka barua hiyo iambatanishwe na katiba na muhtasari wa kikao kilichofanya uamuzi, tunataka aueleze umma agizo lake analitoa kwa mujibu wa kanuni ipi?"
Katika ufafanuzi wake zaidi amesema, "Ndugai kwa mara nyingine tena amesimama bungeni na kuwashambulia viongozi waandamizi wa chama kwa kufanya uamuzi wa ndani wa chama wa kikatiba wa kuwachukulia hatua za kinidhamu wasaliti 19 kwa kuwafukuza uanachama lakini anafanya yote haya kinyume cha Katiba ya kuendelea kuwapa hadhi ya kibunge watu ambao hawana sifa," amesema Moza.
Amesema kuendelea kukumbatiwa kwa wabunge 19 ni sawa na kukashifu na kubeza hatua ya Rais Samia aliyeahidi kukutana na viongozi wa kisiasa kama alivyoeleza wakati akilihutubia Bunge.