Bawacha walaani kuzuiwa mazoezi, RPC Kingai awaonya

Muktasari:

  • Wakati Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) likilaani kitendo cha Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es salaam kuzuia mazoezi waliyofanya jana, leo Septemba 19, Kamanda wa Kinondoni, Ramadhani Kingai amewaonya akisema wasiwabipu.

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) likilaani kitendo cha Jeshi la Polisi  Mkoa wa Dar es salaam kuzuia mazoezi waliyofanya jana, leo Septemba 19, Kamanda wa Kinondoni, Ramadhani Kingai amewaonya wanachama hao akisema Polisi wana akili zaidi yao na kwamba wasiwabipu.

Kupitia taarifa  iliyotolewa kwa umma leo Septemba 19, 2021  na Kaimu Mwenyekiti Bawacha, Sharifa Suleman imeeleza  tukio hilo lilitokea asubuhi ya Septemba 18, 2021 ambapo Polisi hao kiume, walivamia na kusambaratisha mazoezi hayo wakidai kuwa ni "Maandamano Haramu.’’

“Mazoezi haya ni jambo la kawaida ambalo wanawake hawa wamejipangia kufanya kila wiki kwa ajili ya kuimarisha afya zao. Vitendo hivi vimekuwa vinalenga matukio yanayofanywa na Chadema pekee kwani CCM imekuwa inaendelea na matukio mbalimbali ikiwemo Jogging, mikutano ya ndani na hadhara bila kubughudhiwa kwa namna yoyote na Jeshi hilo,” imeeleza taarifa hiyo.

Bawacha imesema kitendo cha Polisi kuzuia mazoezi hayo kwa nguvu kudhalilisha raia na kwamba havitavumiliwa.

“Kila mmoja ana haki ya kuheshimu na heshima na staha. Bawacha itaendelea kuwa ya wanawake wote nchini dhidi ya vitendo vyote vya udhalilishaji na kuonewa.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu malalamiko ya Bawacha leo, Kamanda Kingai amesema hiyo ilikuwa sio Jogging bali wanachama hao walikuwa na nia ya kufanya maandamano ya kimkakati hivyo walichukua maamuzi ya kuvamia na kuwasambaratisha.

“Nitumie fursa hii kuwaonya kwa sababu walichokuwa wanakifanya wao ilikuwa ni nia ya kufanya maandamano Ulishawai kusikia wapi jogging ya chama? Kingine unafanya mazoezi ukiwa umevaa fulana zilizoandikwa tunataka tume huru ya uchaguzi,” amehoji Kingai.

Kingai amesema hiyo sio Jogging bali yalikuwa maandamano ya kimkakati na aliwaonya kuendeleza vitendo hivyo na kwamba wasiendelee kulibipu jeshi hilo kwani wanatakiwa kuzingatia taratibu za kisheria kama zinavyoeleza.