Bei mpya ya dizeli, petroli kivumbi

Muktasari:

  • Kivumbi leo’ hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta Septemba ambazo zimepaa huku maumivu zaidi yakiwa katika bei ya dizeli.

Dar es Salaam. ‘Kivumbi leo’ hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta zitakazotumika Septemba ambazo zimepaa huku maumivu zaidi yakiwa katika bei ya dizeli.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumanne Septemba 5, 2023 saa 4 usiku na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk James Mwainyakule imeonesha kuwa kuanzia leo Jumatano Septemba 6 jijini Dar es Salaam petroli itauzwa Sh3,213 na dizeli itauzwa kwa Sh3,259.

Bei hizo zinamaanisha kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam petroli imeongezeka kwa Sh14 kutoka Sh3,199 ya Agosti huku dizeli ikiongezeka zaidi kwa Sh324.

Hata hivyo kwa upande wa mikoa mingine yenye bandari zinazoshusha mafuta nchini pia bei ya mafuta imepaa; Mtwara kwa mwezi huu lita moja ya petroli itauzwa Sh3,285 ikiongezeka kutoka Sh3,271 na upande wa dizeli itauzwa Sh3,332 kutoka Sh3,008 mwezi uliopita.

Aidha, bei ya mafuta pia imepaa kwa Mkoa wa Tanga ambapo kwa sasa lita moja ya petroli itauzwa Sh3,259 kutoka Sh3,245 Agosti huku dizeli nayo ikiongezeka zaidi kutoka Sh2,981 Agosti hadi Sh3,305.

Wakati hali ikiwa hivo katika mikoa mitatu yenye bandari, pia bei itang’ata zaidi mkoani Kagera katika eneo la Kyerwa (Ruberwa) ambapo petroli itauzwa Sh3,450 kwa lita na dizeli itauzwa Sh3,497.

Kuhusu sababu ya kupanda kwa mafuta, Mkurugenzi wa Ewura amesema gharama za uagizaji katika soko la dunia na maamuzi ya kisiasa wa nchi wazalishaji mafuta zimechochea.

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa Septemba 2023 yanatokana na kupanda kwa gharama katika soko la dunia kwa hadi asilimia 21, gharama za uagizaji wa mafuta hadi asilimia 62 ikilinganishwa na Agosti,”

“Pia, maamuzi ya kisiasa katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC+) imekuwa chanzo,” ameongeza.

Hali kama hii ya kupanda kwa bei za mafuta ilitokea mwaka jana ambapo Serikali Mei 2022 iliweka ruzuku ya Sh100 bilioni katika bidhaa hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi ili kupoza bei yake. Na Januari 2023 iliiondoa ruzuku hiyo.