Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya maji kupanda?

Muktasari:

  • Maji ya kunywa ni miongoni mwa bidhaa zinazotarajiwa kuongezeka bei.

Dar es Salaam. Huenda bidhaa ya maji, ikawa miongoni mwa zitakazopanda bei, iwapo bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/24 itapitishwa.

Matarajio ya ongezeko la bei katika bidhaa hiyo, yanatokana na hatua iliyopendekezwa na Serikali ya kuongeza ushuru maalumu wa asilimia 10 katika bidhaa zisizo za petroli zinazohusisha maji.

Hata hivyo, hatua hiyo imelalamikiwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), wakisema kiwango pendekezwa hakilingani na bei halisi ya bidhaa husika, ikilinganishwa na nyingine kwenye kundi hilo kama soda.

Nyongeza ya ushuru wa asilimia 10 katika bidhaa hiyo, ilipendekezwa na Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Juni 15, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Akiwasilisha hoja hiyo ndani ya bajeti Dk Nchemba alisema: “napendekeza kufanya marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru kwa kiwango cha asilimia 10 ya bei kwenye bidhaa zisizo za petroli na asilimia 20 ya bei kwenye bidhaa za bia na tumbaku,” alisema.

Hata hivyo, pendekezo la nyongeza hiyo litafanya lita moja ya maji itozwe ushuru wa Sh75.2 badala ya Sh58 unaotozwa sasa, ambayo hata hivyo ilikuwa ikilalamikiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchambuzi wa bajeti hiyo, Makamu Mwenyekiti wa CTI, Hussein Sufiani amesema umefika wakati Serikali iangalie upya ushuru unaotozwa katika maji.

Amesema nyongeza hiyo ya ushuru katika bidhaa ya maji imekuja kipindi ambacho hata iliyopo sasa ya Sh58 kwa lita inalalamikiwa.

“Tangu mwaka 2012 tumekuwa tukiomba punguzo katika ushuru wa bidhaa hiyo, tulipendekeza iwe nusu ya Sh58 hii ni kutokana na umuhimu wa bidhaa husika,” amesema.

Hata hivyo, Sufiani amesema katika bidhaa zote zilizojumuishwa kwenye ushuru huo, ikiwemo soda hakuna hata moja yenye bei inayofanana na lita moja ya maji.

Ameeleza lita moja ya maji inayouzwa Sh500 inahusisha gharama nyingine lukuki kama usafirishaji na mambo mengine hivyo ushuru huo utaongeza gharama.

“Wanachama walipeleka ombi kutokana na mwenendo wa biashara walifikiri mabadiliko yoyote yangekuwa na athari kwenye kiwango cha mauzo kwa sababu yatasababisha ongezeko la bei,” amesema.

Kwa hali ilivyo, amesema ni wakati wa Serikali kuangalia upya ushuru maalum katika bidhaa ya maji ya kunywa ili kuleta unafuu kwa wazalishaji.

Pamoja na kupongeza baadhi ya marekebisho katika bajeti hiyo, Sufiani amesema yapo maeneo ambayo Serikali inapaswa kuzingatia ili kurahisisha zaidi mazingira ya biashara nchini.

Ameyataja maeneo mengine ni ushuru wa Sh20 uliopendekezwa kutozwa kwenye kila kilo moja ya saruji.

"Tumepata maoni kutoka kwa wazalishaji wanahisi itachangia kuongeza gharama ya uzalishaji na gharama ya bidhaa, itaathiri upatikanaji, tunaomba Serikali kulifikiria jambo hili," amesema.

Amelitaja eneo lingine ni hatua ya kupunguza ushuru wa asilimia 50 hadi asilimia 35 katika vitenge vinavyoingizwa kutoka nje, akisema itawaathiri wazalishaji wa ndani.

"Katika nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wenzetu bidhaa hii inatozwa asilimia 50 ya ushuru kwa wanaoingiza kutoka nje, basi tunapaswa tufanye hivyo ili kuwapa nafasi wazalishaji wa ndani," amesema.

Kulingana na Sufiani, eneo lingine ni kuendeleza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa mwaka kwenye nyuzi za pamba badala ya asilimia 25 ilivyopendekezwa kwa mujibu wa bajeti hiyo.

"Kuanzisha kodi ya ongezeko la faida kwa asilimia 10 katika mapato yanayotokana na uuzaji wa bidhaa za hewa ukaa," amesema.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa CTI, Leodgar Tenga amesema kinachofanywa na shirikisho hilo ni kutoa tamko kuhusu bajeti ya Serikali.

“Tumekuwa tukifanya hivi mara zote na tumekuwa tukipendekeza mara zote, lakini bajeti hii kwa sehemu kubwa imegusa maeneo tuliyopendekeza,” amesema.